TANESCO KUWAFIKISHA KWENYE VYOMBO VYA SHERIA WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA UMEME KARIAKOO

September 04, 2025


Katika kuhakikisha vitendo vya wizi na uharibifu wa  miundombinu ya umeme vinakomeshwa nchini, TANESCO  itawafikisha katika vyombo vya sheria baadhi ya wafanyabiashara waliobainika kutumia umeme kinyume na  utaratibu baada ya kuchepusha baadhi ya Nyaya kwenye mita ili kuzifanya mita hizo kushindwa kuhesabu umeme unaotumika.


Akizungumza Septemba 03,2025  katika operesheni ya kuwasaka wahujumu wa miundombinu ya umeme katika eneo la Kariakoo mtaa wa Agrey Mhandisi Mohamed Lacha wa  kitengo cha kudhibiti mapato TANESCO alieleza kuwa  matukio kama hayo yanaikosesha  Shirika mapato hivyo  waliohusika na matukio hayo  watafikishwa kwenye vyombo vya sheria  na kusitishiwa huduma ya umeme na kutakiwa kulipa deni wanalodaiwa.


‘’Watu hawa wanatarajiwa kuchukuliwa hatua za kisheria lakini pia sisi kama TANESCO tutawasitishia huduma ya umeme na  watalazimika kulipa deni lote wanalodaiwa kwa muda wote waliofanya vitendo hivyo .‘’alifafanua Mhandisi Lacha


Kwa upnde wake Mhandisi Edson Mwasala alisema, katika operesheni walioifanya  Mtaa wa Mchikichini wamebaini uwepo wa wapangaji kumi na nane ambao kwa upande wao wanachangishwa fedha za kulipa bili ya umeme lakini hakuna fedha inayoingizwa kwenye mita husika baada mita kuchezeshwa.


 Baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo wameiomba TANESCO kuendelea  kufanya msako wa mara kwa mara ili kuwabaini wanaoihujumu miundombinu ya umeme kwa kuwa katika maeneo ya Kariakoo wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekumbwa na kadhia ya kusitishiwa huduma ya umeme kwa makosa ya watu wengine ambao sio waaminifu.


Hata hivyo TANESCO inaendelea na zoezi la kuwasaka wateja ambao wanatumia umeme kinyume na utaratibu ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »