Na Oscar Assenga, TANGA
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Tanga (CCM) Kassim Makubeli amehaidi kwamba endapo atachaguliwa kuwatumikia wananchi atahakikisha anasimamia kwa karibu usanifu na ujenzi wa barabara za Juu (Flyovers) eneo la Kwaminchi kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na ujenzi wa madarasa.
Makubeli aliyasema hayo wakati wa Mkutano wa Kampeni uliofanyika eneo la uwanja wa Komesho Jijini Tanga ambapo alisema licha ya hivyo pia atahakikisha anasimamia miradi mingine ya maendeleo kama ilivyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma
Alisema eneo hilo kuna umuhimu mkubwa kuwa na barabara za juu ili kupunguza msongamano ambao unaweza kujitoeza hasa nyakati wa asubuhi na jioni ambapo wakati mwengine kumekuwa kukishuhudiwa foleni.
Aliwaomba wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura Octoba 29 kuwachagua kwa kumpa kura nyingi Rais Dkt Samia Suluhu na yeye kuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga ili aweze kuwapa maendeleo.
Awali akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman aliwaomba wakazi wa Tanga kumchagua Kasim Amary Makubeli akieleza kwamba atakuwa kiendelezo wa kazi nzuri zilizofanywa na mtangulizi wake Ummy Mwalimu.
Alisema kwamba makubeli ni chaguo sahihi kwa sababu amepewa dhamana na chama kutekeleza ilani ya CCM ambayo msingi wake Mkuu ni amani,maendeleo na mshikamano wa Kitaifa.
Aidha alisema kwamba katika shughuli za maendeleo katika Jimbo hilo kuwa miradi mikubwa ya kimkakati imeanza kutekelezwa ikiwemo upanuzi na maboresho ya Bandari ya Tanga,Ujenzi wa viwanda pamoja na kuimarisha sekta ya elimu kwa kujengwa shule za Sekondari mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Rajabu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alisema kwamba katika sekta ya afya ,Rais Dkt. Samia Suluhu ameendelea kupungumza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwepo awali kwa kujenga Vituo vya Afya,zahanati pamoja na kuboresha Hospitali za Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo.
Aliwataka wana CCM kuendelea kuendesha kampeni za Kistaarabu ili kuwaonyesha wapinzani kuwa CCM kina watu wema.
Naye kwa upande wake Mbunge aliyemaliza muda wake Ummy Mwalimu aliwataka wakazi wa Tanga kumchagua kwa kumpa kura nyingi Mgombea Urais wa CCM Dkt Samia Suluhu na mgombea Ubunge Kassim Makubeli na madiwani wa chama hicho ili kurahisisha maendeleo.
Mwisho.
EmoticonEmoticon