CCM YASIMAMISHA JIJI LA TANGA WAKIFUNGA KAMPENI

October 28, 2025

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mkutano mkibwa wa kufunga kampeni za uchaguzi mkuu kimkoa.

Mkutano huo umefanyika jana Oktoba 27 katika eneo la Comercial na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa jiji hilo na kutoka maeneo mengine ya mkoa wa Tanga.

Mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurhaman.


Mkutano huo pia umehudhuriwa na wagombea wote wa ubunge wa CCM kutoka majimbo 12 ya mkoa wa Tanga, wakiongozwa na mwenyeji wao mgombea wa Jimbo la Tanga Mjini, Kassimu Amari Ambaraka (Anko Makbel).


Wengine walioshiriki ni wagombea udiwani kutoka kata mbalimbali za mkoa wa Tanga, viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM mkoa wa Tanga, wanachama, wananchi na wakereketwa wa chama hicho.


Umati wa wananchi ulianza kujitokeza katika eneo la mkutano kuanzia majira ya saa 8:00 mchana kwa ajili ya kushiriki shamramshamra za  ufungaji wa kampeni hizo, pamoja na kusikiliza hotuba za viongozi hadi shughuli hiyo ilipohitimishwa saa 12:00 jioni.

Mavazi ya njano na kijani yalitawala katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, huku mabango na bendera za chama hicho zikipepea katika maeneo maeneo mbalimbali.

Wasanii mbalimbali, ngoma za asili, vikundi vya hamasa na nyimbo mbalimbali za hamasa za CCM zilipamba ufungaji huo na kuleta ladha ya aina yake.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rajabu amewaomba wananchi wa mkoa wa Tanga kuipigia kura nyingi za ushindi wa kishindo CCM, kwani imetekekeza kwa vitendo ahadi zote ilizotoa katika ilani yake ya uchaguzi iliyopita ya 2020/2025.

Ametaja baadhi ya ahadi zilizotekelezwa na kuleta manufaa makubwa kwa wananchi ni,  uboreshaji wa huduma za kijamii kama ujenzi wa miundombini ya barabara, bandari,  hospitali na vituo vya afya, ujenzi wa shule mpya na madarasa kwa shule za msingi na sekondari, usambazaji wa maji na umeme hadi vijijini, kudumisha amani na utulivu na mengineyo mengi.

Aidha, amesema ilani mpya ya uchaguzi ya 2025/2030 imeahidi mambo mengi makubwa zaidi ya maendeleo, ikiwamo kuendeleza  ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tanga, uboreshaji wa huduma za maji, umeme, afya na elimu na uboreshaji zaidi wa Bandari ya Tanga.

Nae mgombea ubunge Jimbo la Tanga Mjini, Kassimu amewaomba wanachi wa jimbo hilo kumpigia kura nyingi za ndio mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye katika nafasi ya ubunge na wagombea wote wa udiwani wa chama hicho, ili waweze kushirikiana nao kuleta maendeleo makubwa zaidi.

Akitoa taarifa ya CCM mkoa, Katibu wa chama hicho mkoa wa Tanga, Jamal Abasi Kimji amesema chama hicho  kimefanya kampeni zake kwa amani na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Amesema katika kipindi hicho cha kampeni, wagombea wa chama hicho wamewafikia wananchi wengi na kuinadi vyema Ilani ya uchaguzi.

Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unafanyika kesho.

#kazinaututunasongambele

#OktobaTunatiki

#Anko Makbel



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »