Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi, mkoani Singida, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini Wilaya ya Ikungi walipokuwa wakitoa tamko la kuwaomba wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.
.....................................
Na Mwandishi Wetu, Ikungi
VIONGOZI wa Dini Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa
tamko la kuwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo kushiriki kikamilifu kwa Amani
uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.
Tamko hilo wamelitoa Oktoba 27, 2025 wakati wakizungumza
na waandishi habari na kueleza kuwa Oktoba 29 kila baada ya miaka mitano ni siku ya uchaguzi
mkuu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini wenzake Askofu
Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi alisema
wakiwa kama walezi wa maadili, amani na mshikamano katika jamii wanatoa tamko
hilo kuhamasisha wananchi wote wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
“ Kupiga kura ni haki ya kila mtu kikatiba na ni wajibu wa
kizalendo, tunawasihi wananchi wote waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Nyika.
Aidha Askofu Nyika aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya
busara na ya haki kwa kuchagua viongozi wanaoamini watawatumikia kwa uadilifu huku
wakitambua kwamba kura ni haki yao na kulinda amani ya nchi ni wajibu wa kila
mmoja wetu.
Askofu Nyika alisema kudumisha amani ni msingi wa maendeleo
ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo wanawakumbusha wananchi wote kwamba
tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, migawanyiko, maandamano na
vurugu siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na visipewe nafasi kwa sababu
amani ni zawadi kutoka kwa Mungu isichezewe hata kidogo.
“Sisi Viongozi wa dini kutoka Wilaya ya Ikungi tutaendelea kuliomba taifa letu
liendelee kuwa na utulivu, mshikamano, upendo na tunawasihi waumini wetu
waendelee kuiombea nchi yetu ya Tanzania,” alisema Askofu Nyika.
Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani alisema
tunapoenda kupiga kura kesho jambo la kwanza ni kuangalia amani ya nchi
yetu kwani amani ni tamko lililotoka kwa Mungu na ni jambo kubwa sana.
“Tuna wasihi wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa
ujumla kuendelea kuitunza amani hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, “ alisema
Sheikh Selemani.
Sheikh Selemani aliwaomba wananchi wote waliojiandikisha
kupiga kura kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kufanya hivyo kwani ni haki yao na wasipofanya hivyo watakuwa wamejinyima haki hiyo.
Naye Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal
Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi, alisema kesho Oktoba 29, 2025 ni
jukumu la kila Mtanzania aliyejiandikisha kujitokeza kwenda kupiga kura kwa
ajili ya kumchagua Rais wetu, wabunge na madiwani.
“Kwa bahati nzuri vyama vyote vilivyoshiriki kampeni
tumewaona wagombea wao walivyoshiriki kunadi sera za vyama vyao hivyo imetupa
urahisi wa kujua ni nani wa kuweza kutuongoza katika taifa letu hivyo ni wito
wetu viongozi wa dini kwenu kesho Oktoba
29, 2025 mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Samuel.
Viongozi wa dini walioshiriki katika mkutano huo ni kutoka Jumuiya Zawwiyyatul Qaadiriyya Tanzania (JZQT) ambayo,ni muungano wa mazawiyya yote ya Tanzania, Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), The Free Pentecostal Church Of Tanzania, Kanisa la CPCT na Aswar Suna
EmoticonEmoticon