
Watumishi wa Jeshi la Magereza wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwapatia majiko ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wakizungumza leo Agosti 04, 2025 wakati wa hafla fupi ya kupokea mitungi hiyo ya gesi pamoja na majiko ya sahani mbili kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Maafisa pamoja na Askari wa Jeshi hilo wamesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia itawaongezea ufanisi katika majukumu yao.
“Kwanza tungependa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika kuhakikisha Watanzania tunaachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.
Kwa niaba ya Maafisa na askari wa jeshi la Magereza tunapenda kushkuru kwa kupatiwa mitungi ya gesi pamoja na majiko yake. Majiko haya ya gesi yatasaidia watumishi kuongeza ufanisi katika kazi zao,” amesema Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mkuza, SSP. Ibrahim Nyamka huku wakiahidi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.
Awali akizungumza kabla ya ugawaji wa majiko hayo kwa watumishi wa jeshi hilo Mkoa wa Pwani, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Mhandisi Sophia Mgonja ambaye pia alikuwa ameambatana na Mjumbe mwingine, Wakili Msomi Mwantumu Sultan amesema kuwa ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi pamoja na majiko yake ni muendelezo wa jitihada za serikali katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umebainisha kuwa kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mhandisi Godfrey Chibulunje ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo ya nishati safi ya kupikia ili lengo la mkakati huo pamoja na malengo ya nchi yaweze kufikiwa.
Awali akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuele Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 702 yatagaiwa kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Pwani.












EmoticonEmoticon