KAMISHNA BADRU KUENDELEA NA ZIARA YA KATA KWA KATA TARAFA YA NGORONGORO

December 21, 2025


 _Aendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira, uhifadhi shirikishi, kuibua na kuboresha huduma za Kijamii na kupunguza migogoro kati ya Wanyamapori na Binadamu._ 


Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.


Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kupatikana kwa madiwani wapya ndani kwa kata zilizopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Abdul-Razaq Badru ameanza  kufanya ziara ili kukutana na madiwani na wananchi wa tarafa ili ili kuendelea kuimarisha mahusiano, kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa lengo la kuwa na uhifadhi endelevu na maisha salama kwa wananchi.

Badru ameanza ziara yake  katika kata ya Endulen  Jumamosi ya tarehe 20 Desemba, 2025 na kukutana na diwani wa kata hiyo mheshimiwa Dkt. Elias Sakara Nagol ambapo katika mazungumzo yao walijadili namna bora ya kushirikiana ili kuimarisha usimamizi madhubuti wa sheria,upatikanaji wa huduma za kijamii kupitia fedha zinazotengwa na mamlaka pamoja na udhibiti wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.

“Nitahakikisha kila ninapopata nafasi ninapita katika kata zilizopo ndani ya hifadhi ili kukutana na viongozi wenzangu katika ngazi za kata na vijijini ili kuweka mikakati ya jinsi ya kuishi salama na kushirikiana kutatua changamoto zetu kwa pamoja,”alisema bwana Badru.

Katika kata ya Endulen tayari Mamlaka inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji ambao kukamilika kwake kutasaidia kupatikana kwa maji katika baadhi ya vijiji vya kata hiyo ambayo yatasaidia kuondoa adha ya maji kwa binadamu na mifugo. Aidha mamlaka hiyo inasaidia mafuta ya Jenerata katika kata hiyo sambamba na kusomesha watoto wanaotoka familia za kipato cha chini.

Miradi mingine  ya maji inayotekelezwa katika tarafa ya Ngorongoro ni pamoja na uchimbaji wa visima katika kata za Kakesio, Endulen,Nainokanoka na Olbalbal  ambapo kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kwa Kiasi kikubwa kuondoa kero ya maji kwa binadamu na mifugo.


Bi Esupat Saitoti mmoja wa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro amesema kuwa juhudi zinazofanyika hivi sasa za kuboresha huduma na mikutano ya pamoja inasaidia kuondoa migogoro baina ya askari wa mamlaka na wananchi.

“Tunashukuru sana jitihada zinazofanyika hivi sasa ambapo viongozi wa Mamlaka wamekuwa karibu na wananchi na kila tunapowahitaji wamekuwa wakijumuika nasi”,amesema bwana Emmanuel Ole Saitoti Joseph mkazi wa Endulen


Mamlaka pia itashirikiana na TARURA kukabiliana na changamoto ya usafiri kwa kuona namna ya kufanya maboresho ya barabara za ndani ya hifadhi ili ziweze kupitika mwaka nzima  kama ambavyo tayari imeshafanyika kwa barabara ya kutoka Kata ya Ngorongoro, Misigyo, Endulen, Kakesio kuelekea Meatu.


Tarafa ya Ngorongoro ina vijiji 25 vilivyopo ndani ya hifadhi ambapo kukamilika kwa ziara  hiyo  ya kamishna ndani ya maeneo hayo kutasaidia kukumbushana umuhimu wa viongozi, wananchi, wahifadhi na watoa huduma nyingine kufuata sheria  na taratibu ili kuepuka misuguano ya mara kwa mara.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »