………………………..
Na Sixmund Begashe – Butuli Simiyu
Wizara ya Maliasili na Utalii ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda maeneo yanayohifadhiwa kisheria pamoja na kuhakikisha udhibiti wa Wanyamapori hao unafanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo wananchi kuacha kuvamia na kulima mazao yanayopendwa na wanyamapori hususan Tembo pamoja na kuchunga mifugo maeneo ya wanyama hao.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba alipotembelea Kijiji cha Butuli kinachopakana na Pori la Akiba Maswa na kushuhudia namna baadhi ya wananchi wakiendesha shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mpaka na wengine ndani ya eneo lililohifadhiwa Kisheria.
Akiongea na Maafisa na Askari wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), CP. Wakulyamba amesema kuwa Mhe. Waziri Balozi Dkt Pindi Chana ameagiza jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama pamoja na mali zao na hasa kudhibiti vifo vinavyotokana na Tembo.
CP. Wakulyamba ameongeza kuwa Waziri Balozi Dkt. Chana ameagiza kuendelea kujenga mahusiano mema na wananchi wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuhakikisha wanapatiwa elimu ya kutosha, pamoja na kuwashirikisha kikamilifu katika mapambano dhidi ya wanyama hao.
“Sisi wahifadhi tunayafahamu kitaaluma maeneo tunayoyalinda kwa kuwa tumesomea na tumeletwa hapa kufanya kazi lakini Wananchi wanaoyazunguka maeneo ya Hifadhi wao wanayafahamu kwa asili, wamezaliwa hapo, wanaishi hapo hivyo wanayajua kwa undani mkubwa. Tukishirikiana nao watatusaidia hata kuwajua wahalifu dhidi ya maliasili zetu”, Alisema CP Wakulyamba.
Aidha, CP. Wakulyamba amewataka askari hao wa TAWA kuzingatia mafunzo waliyopewa na Maafisa wa Polisi Mrakibu wa Polisi Joseph Jingu na Mrakibu wa Polisi Ocsar Felician sambamba na Afisa Mhifadhi Edwin Nyerembe kutoka Wizara ya Maliasilina Utalii juu ya Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria. Mafunzo hayo ni utekelezaji wa Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotokana na maoni ya Tume ya Jinai.
Mafunzo mengine yanayotolewa na Maafisa hao ni pamoja na matumizi sahii na salama ya Silaha yakilenga kuboresha utendaji kazi ndani ya Jeshi hilo la Uhifadhi.
Awali akitoa Taarifa ya utekelezaji wa shughuli Katika Pori la Akiba Maswa, Kamishna Msaidi wa Uhifadhi Saidi Kabanda, ambaye ni Kaimu Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Ziwa TAWA, amesema moja ya jitihada zilizochukuliwa katika Mkoa wa Simiyu ni pamoja na kujengwa kwa vituo vinne vya kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu, kukarabari vituo vingine vinne pamoja na kuongeza askari wa Uhifadhi na wa Vijiji (VGS).
Naye Afisa mtendaji Kijiji cha Butuli Emmanuel Fabian machibya ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua zinazochukuwa za kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Butuli katika mapambano dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu hali inayoleta faraja zaidi kwa wananchi.
EmoticonEmoticon