MBUNGE MNZAVA AWAKABIDHI WAZEE 300 BIMA ZA AFYA KUPITIA MAKUYUNI FESTIVAL

December 26, 2025

MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mnzava, ameendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wazee kwa kugawa Bima za Afya kwa zaidi ya wazee 300 waliohudhuria Makuyuni Festival, tamasha lililowakutanisha wakazi wa maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mnzava amesema  hatua hiyo inalenga kuhakikisha wazee wanapata huduma bora za matibabu bila vikwazo vya kifedha, huku akisisitiza kuwa afya ya wazee ni sehemu muhimu ya ustawi wa jamii.

 "Bima hizo zitawawezesha wazee kupata matibabu kwa wakati wowote na katika vituo vilivyosajiliwa, hatua inayotafsiriwa kama kupunguza mzigo wa gharama za afya kwa familia nyingi za kipato cha chini."amesema Mhe.Mnzava

Katika tamasha hilo, Mbunge Mnzava pia alipata fursa ya kushiriki chakula cha pamoja na wazee, watu wenye ulemavu, vijana na wananchi wengine waliohudhuria, akisema kitendo hicho ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuonyesha ushirikiano kwa jamii ya jimbo lake.

Amesema Makuyuni Festival ni jukwaa muhimu katika kuwaunganisha wananchi, kubadilishana mawazo na kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za kijamii zinazochochea maendeleo ya Korogwe Vijijini.

Hata hivyo ametumia a nafasi hiyo kuwatakia wananchi wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla heri ya Sikukuu ya Krismasi, akisisitiza umuhimu wa kusherehekea kwa amani, upendo na mshikamano.

Amesema Krismasi ni kipindi cha kutafakari baraka za Mungu na kuonyesha huruma kwa watu wenye uhitaji, akiwahimiza wananchi kuendeleza moyo wa ukaribu na kusaidiana bila kujali tofauti zao.

Mhe. Mnzava amewahimiza vijana na wananchi wote kutumia Sikukuu ya Krismasi kama chanzo cha nguvu mpya na hamasa ya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uzalendo na bidii katika kuchochea maendeleo ya jimbo hilo.

Amesema serikali kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo mbalimbali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo afya, elimu, maji na barabara ili kuhakikisha ustawi wa wananchi unaongezeka.

Aidha Mnzava amewahimiza wadau wote wa maendeleo wa korogwe ambao wanaishi maeneo mbalimbali nchini, kurudi nyumbani kuja kuwekeza ili kuzidi kuinua maendeleo ya korogwe

Kwa upande wao, baadhi ya wazee walionufaika na bima hizo walimshukuru mbunge kwa kuona umuhimu wa afya zao, wakisema hatua hiyo imewapa faraja na matumaini katika kupata matibabu kwa uhakika.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »