MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAFUNGUA FURSA MPYA ZA AJIRA KWA WATANZANIA

December 31, 2025




Imeelezwa kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yameendelea kufungua fursa nyingi za ajira kwa Watanzania, hususani katika uzalishaji wa mkaa mbadala na utengenezaji wa mashine za kuzalishia mkaa huo.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay amesema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Wazalendo Movement inayojishughulisha na utengenezaji wa mashine za kuzalisha mkaa mbadala pamoja na uzalishaji wa mkaa huo wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Bw. Mlay amesema kuwa taasisi nyingi zinazohudumia watu kuanzia 100 na kuendelea zimeanza kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, jambo linaloongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya mkaa mbadala na hivyo kuhitaji uzalishaji wa kasi zaidi.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuzalisha mkaa mbadala pamoja na mitambo ya kutengenezea mkaa huo. Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kwani mahitaji ni makubwa, lakini ni muhimu kuhakikisha mkaa huu unaozalishwa ni wa ubora wa hali ya juu na unaodumu hata ukisafirishwa kwa umbali mrefu,” amesisitiza Bw. Mlay

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Deusdedit Malulu amesisitiza umuhimu wa kushirikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika utengenezaji wa mkaa mbadala ili kuhakikisha bidhaa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, amewahimiza wazalishaji kujisajili kwenye mfumo wa NEST ili kupata fursa mbalimbali na kubainisha kuwa REA ina mpango wa kutoa fursa kwa wananchi katika utengenezaji wa mashine kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kuzalisha mkaa mbadala.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wazalendo Movement,Bw. Saidi Malema amesema kuwa taasisi hiyo, katika kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, imeanzisha kikundi cha nishati safi ya kupikia kinachojihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala unaotengenezwa kutokana na magunzi ya mahindi na nyasi kavu.

Amesema taasisi hiyo hutengeneza mashine za kuzalishia mkaa zinazotumia umeme na zisizotumia umeme.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia imeanzisha kikundi cha Nishati Safi Sanaa Group, kinacholenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia sanaa ya maigizo na nyimbo.

Amesema Taasisi ya Wazalendo Movement imefanikiwa kuuza mashine zake kwa wadau katika mikoa ya Tabora, Singida na Pwani. Aidha, imekuwa ikigawa mashine ndogondogo kwa wananchi wa vijiji vya Wilaya ya Mkuranga ambako umeme bado haujafika ili kuwahamasisha kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katika ziara hiyo, Bw. Nolasco Mlay pia alitembelea kampuni ya Matima Investment inayojishughulisha na utengenezaji wa majiko ya kuchomea nyama yanayotumia gesi, kwa lengo la kujionea namna majiko hayo yanavyosaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »