PEPFAR YAUPONGEZA MKOA WA TANGA KWA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA VVU

August 30, 2024

 




Na Oscar Assenga, KOROGWE


JUMLA ya vijana 134 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 wamejiandikisha kwenye kliniki ya tiba na matunzo ya VVU katika Hospitali ya Mji wa Korogwe huku asilimia 90 ya vijana hao wakifanikiwa kufubaza makali ya VVU.

Hayo yalibainishwa wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani Tanga walipotembelea hospitali ya wilaya ya Korogwe (Magunga)na Kituo cha Afya cha St.Raphael  vinayowezeshwa na Shirika la THPS kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PERFAR), kupitia Kituo cha Kudhibiti  na Kuzuia Magonja cha Marekani (U.S. CDC).

Kwa mujibu wa Kaimu Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI (RACC) mkoani Tanga, Bi. Judith Kazimoto, THPS kupitia mradi wa Afya Hatua, kwakushirikiana na timu za usimamizi wa Afya za Mkoa na Wilaya, wanatekeleza afua mbalimbali za kupambana na VVU, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana katika vituo 67 vya afya vilivyopo mkoani humo, ikiwemo Hospitali ya Mji wa Korogwe.

Ili kuhakikisha huduma bora za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kina mama wajawazito wanaoishi na VVU hupatiwa huduma zote muhimu, na mara baada ya kujifungua, Watoto wao husajiliwa na kuchukuliwa vipimo vya VVU mapema.

Kupitia mradi wa Afya Hatua, watoa huduma katika kituo cha Afya cha St. Raphael huhakikisha usajili wa Watoto hao unafanyika na wanachukuliwa sampuli za damu ili kufanyiwa kipimo cha VVU ndani ya wiki sita baada ya kuzaliwa kwao na kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki.

“Kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai 2024, jumla ya wapokea huduma za VVU wajawazito 26 walijifungua katika kituo hicho. Watoto waliozaliwa na kina mama hawa walisajiliwa ndani ya siku saba baada ya kujifungua. Kati ya hao, 24 (93%) walichukuliwa vipimo na wote (100%) na matokeo yalionesha wote walizaliwa bila maambukizi ya VVU”, alisema Bi. Kazimoto.

Katika kipindi cha miaka 21 iliyopita, serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) imewekeza zaidi ya dola bilioni 7 nchini Tanzania kwa ajili kukabiliana na janga la VVU. 

Kwa mujibu wa Mratibu wa PEPFAR nchini Tanzania, Bi. Jessica Greene, PEPFAR ilipoanza kazi hapa Tanzania, mwaka 2003, kulikuwa na watu wasiozidi 1,000 tu ambao waliokuwa kwenye matibabu ya VVU.  

“Hivi sasa, PEPFAR inasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 waliopo kwenye huduma ya tiba na matunzo.  Vifo vinavyotokana na UKIMWI nchini vimepungua kwa 76% na maambukizi mapya yamepungua kwa 58%, tangu 2003”, alisema Bi. Greene.

Bi. Greene alisema ingawa lengo la kutokomeza VVU/UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ni kubwa lakini linaweza kufikiwa. 

“Serikali ya Marekani inajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika jitihada za kufikia malengo ya UNAIDS 95-95-95 ifikapo mwaka 2025, ambayo yanalenga 95% ya watu wanaoishi na VVU kufahamu hali zao, 95% ya waliogundulika kuwa na VVU wapate matibabu, na 95% ya wale walio kwenye matibabu waweze kufubaza VVU”, alisema. 

 Utafiti wa hivi karibuni wa Athari za VVU Tanzania 2022-2023 (Tanzania HIV Impact Survey 2022-2023) umeonesha kuwa jitihada za kupambana na VVU mkoani Tanga zimefanikisha kufikia viwango vya juu vya kufubaza VVU kwa 93.5%. 

“Tunaupongeza mkoa ya Tanga kwa hatua hii nzuri na tunaamini wataendelea kudumisha mafanikio hayo tunapoelekea kuyafikia malengo ya UNAIDS 95-95-95”, alisema Bi. Greene







Share this

Related Posts

Previous
Next Post »