KAMPUNI YA TRUMARK YATOA ZAWADI YA EID EL-FITR KWA WATOTO YATIMA JIJINI DAR ES SALAAM

June 27, 2017

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo akizungumza na wanahabari wakati wa kutoa zawadi kwa watoto Yatima wa Kituo cha Mtoto Wetu Tanzania jijini Dar es Salaam leo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo akiwa amekaa na watoto wa kituo hicho.
 Mratibu wa Miradi wa Kampuni hiyo, Gasparino Haule akiongoza kucheza katika hafla hiyo.
 Ofisa  Rasilimali Watu wa Kampuni hiyo, Grace Zikwaze, akizungumza na watoto hao.
 Keki maalumu ya hafla hiyo ikikatwa kwa pamoja. Kushoto ni Makamu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Theobald Truphone na katikati ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo. Wengine ni maofisa wa Kampuni ya Trumark.
 Zawadi zikitolewa.
 Mwanafunzi Shafii Hassan wa kituo hicho akizungumza 
kwenye hafla hiyo.
 Mwanafunzi Wanswekula Zacharia akizungumza na wanahabari kuhusu changamoto walizonazo.
 Nguo zikiandaliwa tayari kukabidhiwa watoto hao.
 Keki maalumu kwa ajili hayo iliyotolewa na Kampuni hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo akiwalisha keki watoto hao.
 Watoto wakiserebuka.
 Ofisa Utawala wa Kampuni hiyo, Azavery Phares akimkabidhi keki hiyo maalumu, mtoto Godwin Steven.
 Picha ya pamoja kabla ya kuicharanga keki hiyo tayari kwa kuila.



 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo akiwa na watoto wake kwenye hafla hiyo.



Na Dotto Mwaibale

JAMII imetakiwa kujenga moyo wa kusaidia watu waliopo katika makundi yenye uhitaji ili nao wajisikie kama watu wengine waliopo katika familia.

Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark inayojishughulisha na uwezeshaji  jamii, Agnes Mgongo wakati kampuni hiyo  ilipokuwa ikitoa zawadi ya Sikukuu ya Eid El-Fitr katika Kituo cha watoto Yatima  cha Mtoto Wetu Tanzania kilichopo Kimara Suca jijini Dar es Salaam leo hii.

"Ni vizuri jamii ikajenga tabia ya kuwakumbuka watoto na watu wengine waliopo  katika makundi maalumu kwa kuwafariji badala ya kuiachia serikali ambayo ina mambo mengi ya kufanya" alisema Mgongo.

Alisema kampuni yake iliguswa na changamoto walizonazo watoto waishio katika kituo hicho ikaona ni vizuri katika kipindi hiki cha sikukuu ya Eid El-Fitr wakajumuike nao kwa kula na kucheza pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali.

Mgongo alitaja zawadi walizotoa kupitia wadau wengine marafiki wa taasisi hiyo kuwa ni nguo, vinywaji na chakula ambacho kilipikwa katika kituo hicho.

Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo watoto waliopo katika makundi yenye  uhitaji, Wanswekula Zacharia alisema ni pamoja na vitabu, karo, sare za shule na  mahitaji mengine.

Alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo mwanafunzi anapaswa kujua wajibu wake akiwa shuleni ni kusoma na si vinginevyo.

Alisema kupokea misaada ni jambo moja lakini hata mtu kufika tu kituoni hapo na  kuwajulia hali bila ya kuwa na kitu chochote ni jambo la heri kwani wanachohitaji  zaidi ni kujumuika na jamii na kupata faraja.

Mwanafunzi wa kidato cha sita, Shafii Hassan ambaye analelewa katika kituo hicho  tangu akiwa mdogo anasema misaada wanayoipata imekuwa ikiwafanya wapate faraja  ukizingatia ukubwa wa changamoto walizonazo.

Makamu Mkurugenzi wa Kituo hicho,Theobald Tryphone aliishukuru kampuni hiyo kwa  msaada huo na kueleza changamoto kubwa walizonazo ni ada za wanafunzi, chakula,  ulipaji wa umeme na kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) wameweka alama za x  katika majengo yao waondoke lakini suala hilo linashughulikiwa na Manispaa ya  Ubungo kuona jinsi itakavyowasaidia kuwasaidia kupata eneo jingine kwa ajili ya 
kujenga kituo hicho.

Mtoto analelewa katika kituo hicho, Godwin Steven alitoa shukurani kwa kampuni  hiyo kwa niaba ya wenzake kwa msaada huo.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »