NAIBU WAZIRI WA MICHEZO AHUDHURIA MCHEZO WA KUMUENZI MCHEZAJI WA MBAO FC ALIYEFARIKI UWANJANI

January 14, 2017
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Annastanzia Wambura, jana akizungumza kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Mhe.Nape Nnauye, kwenye mchezo wa hisani kati ya timu za UMISETA wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza, uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Na Binagi Media Group
Mhe.Wambura, alisema Serikali haijayafuta mashindano ya UMITASHUMITA na UMISETA na kwamba imejipanga vyema ili kuiendeleza michezo hiyo mwaka huu 2017 kwa kuondoa dosari zote zilizojitokeza hapo awali na kusababisha kuahirishwa mwaka jana.

Lengo la mchezo huo ilikuwa ni kumuenzi aliyekuwa mchezaji wa timu ya soka ya vijana chini ya miaka 20 ya Mbao Fc inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Isamail Khalifan Mrisho ambaye Disemba 04 mwaka jana, alifariki dunia akiwa uwanjani kwenye mchezo baina ya na timu yake na Kagera Sugar huku kiingilio kilichopatikana kwenye mchezo huo kikiwasilishwa kwa familia ya mchezaji huyo.

Mchezo huo uliandaliwa na taasisi ya soka nchini iliyomlea mchezaji huyo ya The Football House kwa ushirikiano wa karibu na taasisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mama Angelina Mabula iitwayo Angeline Foundation.

Hadi dakika 90 zinatamatika, timu ya kombaini ya Nyamagana iliibuka mshindi kwa ushindi wa mabo2-1. Mabao ya Nyamagana yalifungwa na Rajesh Kotecha na Kuzaifa Mdabiru huku Ilemela wakipata bao la kufutia machozi baada ya mchezaji wa Nyamagana Jefta John kujifunga.
Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Dkt.Leonald Masele, alisema wilaya yake imejipanga kuhakikisha inaendeleza mchezo wa soka ambapo imeanzisha timu kwa kila soko la machinga wilayani humo hatua ambayo itasaidia kuukuza mchezo huo.
Mkurugenzi wa taasisi ya The Football House, Mbaki Mutahaba, alisema taasisi hiyo itaendelea kumuenzi mchezaji wake Ismail Khalifan Mrisho huku akiwasisitiza vijana kutumia vyema vipaji walivyonavyo kama ilivyokuwa kwa Mrisho ambaye ameacha alama ya soka nyuma yake baada ya umauti kumkuta.
Kaka wa marehemu Ismail Khalifan Mrisho, aitwaye Athman Kitwana, akitoa salamu za shukurani kwa niaba ya familia kwa namna ambavyo wadau mbalimbali walivyojitoa kumwendeleza kipaji chake, kusaidia kwenye msiba wake na namna wanavyoendelea kumuenzi baada ya umauti.
Wazazi wa marehemu Ismail Khalifan Mrisho, kushoto ni  Rehema Mfaume (mama) na kulia ni Khalifan Mrisho (baba). 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »