HALIMA MDEE KUWAONGOZA WANAWAKE SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

March 02, 2015

MWENYEKITI wa Taifa  baraza la Wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Halima Mdee, anatarajiwa kuwaongoza wanawake siku ya wanawake Duniani mjini hapa pamoja na kuzindua matawi  mapya ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mwenyekiti  wa Bawacha Wilaya ya Tanga, Gress Joseph, alisema siku hiyo pamoja na mambo mengine Mdee atazindua matawi na kutoa kadi kwa wanachama wapya.

Alisema siku hiyo Chadema itaitumia kwa  kuwaelimisha wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za kuongoza  na kuacha woga na kuwa mstari wa mbele  kuweza kutetea maslahi yao.

Alisema kuna baadhi ya wanawake wako na uwezo wa kuongoza lakini bado hawajawa na utayari wa kufanya hivyo jambo ambalo limechangia kwa kiwango kikubwa wanawake kuwa nyuma katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Siku ya wanawake Duniani Tanga itazidi kunogeshwa na wabunge wengi wanawake akiwemo Halima Mdee----atatoa misaada katika vituo vya watoto wanaoishi mazingira hatarishi” alisema na kuongeza

“Haitoshi pia atazindua  matawi mapya ya Chadema na kutoa kadi kwa wanachama wapya katika mkutano wa hadhara ambao utafanyika kata ya Nguvumali” alisema Gress

Alisema kwa sasa taratibu zote zikiwemo za  kibali cha mkutano zimeshafanyika na hivyo kuwataka wakazi wa jiji la Tanga kukiunga mkono chama hicho ili kuweza kushika nafasi za kuongoza katika uchaguzi wa Wabunge na Urais.

Kwa upande wake, Katibu wa Bawacha Wilaya, Amina Mahmood, aliwataka vijana kujiunga na chama hicho kwani ndicho ambacho kitaweza kuwakomboa katika  dimbwi la umasikini uliowajaa.

Alisema hali ya maisha ya  Mtanzania imekuwa ngumu huku Serikali ikiwabana katika nyanja mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na hivyo kuwataka kukiunga mkono ili kukiweka kando chama kilicho madarakani..

Alisema utitiri wa kodi zimekuwa kikwazo cha maendeleo na kusema kuwa hakuna chama chochote ambacho kitaweza kuzikomesha zaidi ya Chadema kwani kiko na dhamira ya kweli ya kumkomboa Mtanzania.

“Chadema kila siku kimekuwa kikipiga kelele za kuwaelisha wananchi kukiunga mkono  kwani ndicho  kinachoweza  kuwapunguzia mzigo wa kodi na makali ya maisha” alisema Amina

Alisema mwaka huu Chadema imedhamiria kuchukua viti vya Udiwani na Ubunge jimbo la Tanga kwa kufanya mikutano ya uhamasishaji mjini na vijijini ikiwemo kufungua matawi na kuunda timu moja ya ushindi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »