TIMU TATU FDL ZARUDI LIGI YA MKOA
Timu tatu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitacheza
Ligi ya Mkoa katika mikoa yao msimu ujao baada ya kushika nafasi za mwisho
katika makundi yao, hivyo kushuka daraja.
Transit Camp imekata nafasi ya mwisho katika A
wakati Mkamba Rangers imeshuka daraja kwa kukamata mkia katika kundi B. Nayo
Pamba SC imerudi kucheza Ligi ya Mkoa wa Mwanza baada ya kuwa ya mwisho kwenye
kundi C.
Timu zilizopanda daraja kutoka FDL kwenda Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) msimu ujao ni Ndanda SC ya Mtwara kutoka kundi A, Polisi
Morogoro ya kundi B na Stand United ya Shinyanga iliyoibuka kinara katika kundi
C.
AZAM, YANGA KUTIMULIANA VUMBI VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 9 mwaka huu) huku timu za
Azam na Yanga ambazo zipo nafasi mbili za juu zikiendelea kuchuana.
Azam
itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa
Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani. Nayo Yanga itakuwa mwenyeji wa Kagera
Sugar katika Uwanja wa Taifa jijini.
Yanga,
Azam, Ruvu Shooting na Kagera Sugar zote zimeshinda mechi zao za raundi ya 23
wakati mechi za kesho zitakuwa kwa ajili ya kukamilisha raundi ya 24 ya ligi
hiyo ambayo inatarajia kukamilika Aprili 19 mwaka huu.
Ligi hiyo
itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa
viwanjani. Aprili 12 mwaka huu itakuwa Mtibwa Sugar vs Ruvu Shooting (Manungu,
Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu (Mkwakwani, Tanga), na Tanzania Prisons vs
Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).
Aprili 13
mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Kagera Sugar (Mkwakwani, Tanga), Simba vs
Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mbeya City vs Azam (Sokoine,
Mbeya) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).
TFF YAAFIKA UAMUZI WA KAMATI YA
MAADILI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekubaliana na uamuzi uliofanywa na Kamati
ya Maadili katika malalamiko mawili ambayo iliyawasilisha mbele yake, hivyo
haitakata rufani.
Katibu
Mkuu wa TFF aliwasilisha mashauri mawili mbele ya Kamati hiyo iliyoongozwa na
William Erio. Malalamiko ya kwanza yalikuwa dhidi ya waamuzi wenye beji za
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Oden Mbaga na Samwel Mpenzu na wakufunzi wa waamuzi Riziki Majala na Mchungaji
Army Sentimea.
Wote aliwalalamikia kwa kuwafanyisha mitihani
(wakufunzi), na waamuzi kufanya mitihani hiyo kinyume na utaratibu pamoja na
kughushi matokeo.
Kamati katika uamuzi wake iliiagiza waamuzi hao
kufanya upya mtihani huo katika robo inayofuata ambapo wakifaulu waendelee
kuchezesha mechi. Waamuzi wa FIFA hufanya mitihani hiyo mara nne kwa mwaka.
Kwa upande wa shauri dhidi ya Ofisa Takwimu wa TFF,
Sabri Mtulla ambaye alilalamikiwa kwa kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi dhidi ya mchezaji Emmanuel Okwi, Kamati
iliagiza suala hilo liwasilishwe upya pamoja na ushahidi wa kuthibitisha
malalamiko hayo.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon