KATIBU MKUU MAFUTA NA GESI ASILIA AHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

April 21, 2026




📌Asema ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2050


📌Aeleza  miradi ya kimkakati ya umeme inaongeza uzalishaji  wa umeme nchini


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi asilia, Dkt. James Mataragio, ametoa wito kwa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2050 inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ambayo ni  salama na endelevu.


Dkt. Mataragio ametoa kauli hiyo Aprili 21, 2026, alipotembelea banda la TANESCO eneo la nishati safi ya kupikia kwa umeme , katika maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.


Amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwa ni pamoja na umeme, ili kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla, Aidha, ameipongeza TANESCO kwa juhudi zake za kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutumia umeme kupikia.



‘’ Bajeti ya Nishati inatarajiwa kusomwa Bungeni, miongoni mwa mambo tunayotekeleza katika Bajeti yetu ni Dira ya Taifa ya mwaka 2050 ,hapo kuna kipengele cha nishati safi ya kupikia na kwa ujumla Taasisi zetu ikiwemo TANESCO  zinahamasisha matumizi ya nishati  safi ya  kupika kwa umeme,’’alifafanua Dkt Mataragio.


Kwa upande wake, Mbunge kutoka  Manyara, Mhe. Justina Rahhi, amesifu teknolojia ya majiko ya umeme yanayotumia nishati kidogo, akieleza kuwa yana uwezo wa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.

“Nimejifunza kuwa majiko haya yanatumia umeme kidogo sana ukilinganisha na mkaa. Ni muhimu teknolojia hii iwafikie wananchi wa vijijini ili waweze kunufaika na matumizi ya nishati safi,” amesema Mhe. Rahhi

Naye Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Ruvuma, Mhe. Mariam Nyoka, amepongeza kuimarika kwa huduma ya umeme katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, akieleza kuwa hali hiyo itasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi.



Katika maonesho hayo ya Wiki ya Nishati, TANESCO pia imewasilisha teknolojia mpya ya magari yanayotumia umeme, ambayo yanaelezwa kuwa na gharama nafuu zaidi kwa matumizi ikilinganishwa na magari yanayotumia nishati nyingine.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »