DC RWEYMAM AWAPA SOMO WAZAZI TANGA.

September 28, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweymam amewataka wazazi na walezi Mkoani hapa kuchangia kupatikana kwa unywaji wa maziwa shuleni ili kulinda afya na uelewa wa wanafunzi darasani.

Akizungumza katika siku ya unywaji wa maziwa Duniani na kufanyika kitaifa Mkoani Tanga, Rweymam alisema kinywaji hicho ambacho pia ni chakula ni muhimu kwa faida ya wanafunzi hasa kujenga afya zao.

Alisema wazazi wako na wajibu wa kuona kwa dhati unywaji wa maziwa shuleni ni muhimu na hivyo kuwataka kuchangia ili kuwezesha upatikanaji wa maziwa sambamba na uji shuleni.

“Ni jukumu la wazazi na walezi kuona unywaji wa maziwa shuleni ni muhimu ---mimi nadhani ni jukumu letu sisi wazazi kuwezesha upatikanaji wa maziwa na tusiwe na uzioto wa jambo hilo” alisema Rweymam

Rweymam alisema kufanya hivyo kutawawezesha wanafunzi kuwa na afya nzuri na kuzidisha uelewa darasani lengo ni kuwa na vijana wenye vipaji ambao watakuwa msaada kwa taifa.

Akifunga maadhimisho hayo, Naibu Meya wa jiji la Tanga, Muzzamilu Shemdoe, aliwataka wanafunzi kujibidiisha na masomo yao darasani pamoja na kuacha utoro jambo ambalo linaweza kuwaathiri na maisha mbeleni.

Alisema kuna baadhi ya wanafunzi wamekuwa hawafiki mashuleni mbali ya kuondoka majumbani kwao kuaga kwenda shule hali ambayo baadhi ya shule imekuwa ikikabiliwa na changamoto hiyo.

“Leo ni siku ya unywaji wa maziwa Duniani na kitaifa ni hapa tulipo---sisi tuliopo tu we mabalozi wa elimu majumbani na mitaani kwetu na tuhakikishe kila mtoto anakwenda shule na kuacha utoro” alisema Shemdoe

Shemdoe alisema halmashauri ya jiji inatarajia kufanya kampeni ya kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule haki hiyo anaipata na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka shule watoto wao na kupata elimu.

                                            

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »