8 Januari, 2026
Hayo yamesemwa leo tarehe 08 Januari, 2026 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu – ADEM Dkt. Maulid J. Maulid alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya Utawala Bora wa Elimu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa yanayoendeshwa na ADEM kwa Maafisa Elimu Kata 101 wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha Maafisa Elimu Kata kusimamia kwa ufanisi shughuli zote za elimu katika ngazi ya Kata.
Dkt. Maulid amesema, Maafisa Elimu Kata wana wajibu wa kusimamia kikamilifu shughuli zote za elimu katika ngazi ya Kata hususani usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kushirikiana na walimu wakuu pamoja na viongozi wengine wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambao pia wameshapatiwa mafunzo hayo katika awamu zilizopita hivyo kuwafanya wote kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu uongozi na usimamizi wa shule.
“Uongozi ni wajibu, baada ya kupatiwa mafunzo haya, mna wajibu wa kwenda kusimamia kikamilifu shughuli za elimu katika ngazi ya Kata. Tuone matokeo kuanzia kwenye ngazi ya Shule kwa kwenda kutekeleza kwa vitendo yale mliyojifunza kwenye mafuzo haya. Mahiri mlizojifunza ziwe dira ya kuwasaidia kufanya usimamizi fanisi wa shughuli za elimu katika ngazi ya Kata na ili lengo la Serikali la kuimarisha usimamizi wa sekta ya elimu kuanzia katika ngazi ya shule lifanikiwe”. Amesema Dkt. Maulid.
Aidha, Dkt. Maulid amesisitiza Maafisa Elimu Kata kutambua, kusoma, kuelewa na kutekeleza miongozo yote inayotolewa na Mamlaka zinazosimamia elimu nchini ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Kamishna wa elimu ili iwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa shughuli za elimu.
Vilevile Dkt. Maulid amewataka maafisa hao kuendelea kujifunza, ili kufahamu zaidi kuhusu mabadiliko na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu ili kufahamu wajibu wao katika kusaidia utekelezaji wa maboresho yaliyofanyika.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Dkt. Lucas Mzelela amesema washiriki wa mafunzo hayo wamejengewa uwezo katika maeneo ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu, Utawala Bora katika Elimu, Uandaaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Elimu Ngazi ya Serikali za Mitaa, Ufuatiliaji na Usimamizi Fanisi wa Shule, Usimamizi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Shule, Ukaguzi wa Ndani, na Ushirikishwaji wa Jamii na Utatuzi wa Malalamiko katika Elimu.
Dkt. Mzelela pia amesema kuwa, ni dhahiri kwamba, maeneo hayo yaliyowezeshwa yatasaidia kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule kwa ufanisi.
Mafunzo ya Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yamefanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 6 - 8 Januari 2026 ADEM Bagamoyo na yamefadhiliwa na mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na yatafanyika pia kwa Maafisa Elimu Kata wa Mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Songwe, Rukwa, Katavi, Geita, Ruvuma na Manyara







EmoticonEmoticon