Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, wakati wa uzinduzi wa Tawi la CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Agosti 18, 2026.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda (kulia) baada ya kufungua rasmi Tawi la Benki ya CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Agosti 18, 2026.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda akikata keki wakati akifungua rasmi Tawi la Benki ya CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Agosti 18, 2026.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 ukiwa katika Benki ya CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, wakati wa uzinduzi wa tawi hilo, Agosti 18, 2026.
Wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakifurahia wakati wa uzinduzi wa Tawi la CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 ukiondoka katika Tawi la Benki ya CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, baada ya uzinduzi wa tawi hilo, Agosti 18, 2026.
Na Kadama Malunde & Elizabeth Cosmas Shinyanga
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 umezindua rasmi Tawi la Benki ya CRDB Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, huku benki hiyo ikiahidi kuongeza fursa za huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wastaafu, vijana na wananchi wengine katika eneo hilo.
Tawi hilo limezinduliwa leo Jumanne, Agosti 18, 2026, na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ambaye ameridhishwa na uwekezaji huo akieleza kuwa utaongeza upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi wa Maganzo na maeneo jirani.
Mwang’onda ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na kufanya taasisi za fedha, ikiwemo CRDB, kuendelea kupanua huduma zake nchini.
Amesema mazingira hayo yameiwezesha CRDB kuendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali na kutoa huduma zinazolenga kuchochea shughuli za kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo.
“Awali ya yote nipende kuishukuru Serikali yetu chini ya kiongozi wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki katika Benki yetu ya CRDB, kwani kupitia uwekezaji huo benki hii haina mikwamo tena katika kuwahudumia Watanzania kwa ujumla na wananchi wa Maganzo hii leo,” amesema Mwang’onda.
Aidha, Mwang’onda ameipongeza CRDB kwa kuona fursa ya biashara na kufungua tawi hilo Maganzo, akisema benki hiyo imekuwa ikipanua huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini pale inapobaini mahitaji ya wananchi.
Ameeleza kuwa uwepo wa tawi hilo ni fursa muhimu kwa wakulima, wafanyabiashara na wananchi wengine kupata huduma za kifedha karibu na maeneo yao, ikiwemo mikopo na huduma nyingine zitakazosaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Mwang’onda pia amewataka wananchi kuendelea kutumia huduma za CRDB, akieleza kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa fursa mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo mikopo ya kilimo na uwezeshaji wa shughuli za uzalishaji.
“Niendelee kumpongeza Mkurugenzi wa Mikopo kwa kuendelea kutoa mikopo rafiki kwa wateja, lengo kuu ni kuhakikisha wateja wake wanapata huduma zenye ubora wa hali ya juu,” amesema.
Amesema Serikali pia imeendelea kuweka fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi, huku CRDB ikiwa miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika kuwawezesha wananchi kupitia huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, amesema uzinduzi wa tawi hilo utafungua fursa mbalimbali za huduma za kifedha kwa wananchi wa Maganzo na maeneo jirani.
Makwi amesema kupitia tawi hilo huduma za CRDB zitapatikana kwa urahisi zaidi na kwa kasi, huku wakulima na wafugaji wakipata fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.
“Kupitia tawi hili fursa mbalimbali zitapatikana hapa, huduma zetu zimemulikwa, zitakuwa na kasi zaidi. Kutakuwa na fursa kwa wakulima na wafugaji ambapo mikopo itapatikana,” amesema Makwi.
Amesema pia tawi hilo litawahudumia wastaafu kwa kuwawezesha kuhifadhi fedha zao kwa usalama na kutumia huduma mbalimbali za benki, hivyo kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza endapo fedha zitahifadhiwa bila kutumia mfumo rasmi wa kibenki.
Makwi amewaalika wananchi wa Maganzo na maeneo jirani kufungua akaunti CRDB na kutumia huduma zinazotolewa na benki hiyo ili kunufaika na fursa mbalimbali za kifedha.
“Tunawashukuru sana wananchi kwa kuendelea kutumia huduma zetu,” amesema.
Tawi la CRDB Maganzo limejengwa kwa lengo la kuimarisha huduma za kibenki na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wateja wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo hilo.
Shughuli hizo ni pamoja na uchimbaji na uuzaji wa madini, kilimo cha zao la pamba, nyanya na mazao mengine ya chakula, ufugaji wa ng’ombe na mbuzi, pamoja na shughuli zinazohusiana na biashara na usafirishaji wa bidhaa na abiria.
Ujenzi wa Tawi la CRDB Maganzo umegharimu takribani Shilingi milioni 700, fedha zilizotumika kwa ajili ya ununuzi wa ardhi, ujenzi wa jengo na vifaa.
Wananchi wa Maganzo wameishukuru Benki ya CRDB kwa kufungua tawi hilo katika eneo lao, wakisema kusogezewa huduma za kibenki karibu kutawarahisishia kupata huduma bila kusafiri umbali mrefu.
Wamesema uwepo wa tawi hilo utaongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara, ikiwemo kupata mikopo na huduma nyingine za kifedha, huku wakiahidi kutumia fursa hizo kukuza shughuli zao za kiuchumi.





































































EmoticonEmoticon