


HABARI NA MATUKIO MBALIMBALI








Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Paul Christian Makonda kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Patrobas Paschal Katambi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Richard Stanslaus Muyungi kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhandisi Cyprian John Luhemeja kuwa Balozi kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ndugu Waziri Rajab Salum kuwa Balozi kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026.


Viongozi Wateule wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Januari,2026




Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, amesema ana mpango wa kujenga eneo maalumu litakalofanya kazi kama kijiji cha wanawake kwa ajili ya kuwakutanisha wanawake wafanyabiashara katika sehemu moja ili waweze kuuza bidhaa zao kwa pamoja.
Mavunde ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Januari 12, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanawake kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa wanawake waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi kupitia Chuo cha Veta, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Amesema kijiji hicho kitatoa fursa kwa wanawake kufanya biashara katika mazingira rafiki, kubadilishana uzoefu pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zao, hali itakayosaidia kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
“Lengo letu ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa vitendo, ndiyo maana tunapanga kuwa na eneo maalumu litakalowaunganisha wanawake wote wanaojishughulisha na biashara mbalimbali,” amesema Mavunde.
Aidha, amewataka wanawake wa Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo mafunzo ya ufundi, mikopo na miradi ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wao, wanufaika wa mafunzo hayo wamesema vitendea kazi walivyokabidhiwa vitawawezesha kuanza na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi, huku wakimshukuru Mavunde na Serikali kwa kuwapa mafunzo na msaada unaowawezesha kujitegemea.
“Tunashukuru kwa mafunzo na vitendea kazi hivi, sasa tuna uhakika wa kuanza kujipatia kipato na kusaidia familia zetu,” amesema Boke Ramadhan
Naye Sylvia Mpanda amesema kuwa wangetamani eneo watakalojengewa basi liwe la mjini ili wawapate wateja wengi kutoka maeneo mbalimbali kwani wateja wengi wanapatikana maeneo yenye watu wengi
"Sisi tutafanya kazi kwa kikundi hivyo kwenye hichi kijiji atakachoanzisha Mhe Mavunde kitakuwa na wanawake wengi hivyo niwatake wanawake wengine kuacha kulala majumbani na waje kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali yetu." Amesema Sylvia



Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kutokana na uwepo wa vyanzo vingi vya nishati ya jotoardhi, Tanzania inayo fursa ya kuviendeleza vyanzo hivyo ili wananchi wapate nishati ya kutosha, nafuu na endelevu ikiwa pia ni sehemu ya kuunga mkono malengo ya dunia ya kuelekea kwenye uzalishaji wa umeme unaotokana na nishati safi.
Akizungumza kwenye Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) katika Mkutano wa Mwaka wa Muungano wa Kimataifa wa Jotoardhi (Global Geothermal Alliance – GGA), unaofanyika Jijini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Waziri Ndejembi amesema Serikali imeweka mipango ya uzalishaji wa umeme wa jotoardhi katika Dira ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) na Mkataba wa Nchi kuhusu Masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (NDCs).
Amesema Tanzania pia kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele ya jotoardhi ikiwemo Ngozi (MW 70), Songwe (MW 5–38), Kiejo-Mbaka (MW 60), Natron (MW 60) na Luhoi (MW 5), huku lengo likiwa ni kuwa na mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme wa megawati 130 ifikapo 2030 ambapo mtambo huo utaanza kwa kuzalisha megawati 30.
Katika Mkutano huo, Waziri Ndejembi amealika wawekezaji nchini akieleza kuwa Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuimarisha mifumo ya kisheria na kanuni ili kutoa uhakika wa uwekezaji, kuboresha michakato ya kupata leseni na vibali pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa data za jotoardhi.
Aidha, ili kuweza kuiendeleza ipasavyo nishati ya jotoardhi Ndejembi amesema bado kunahitajika mikopo ya riba nafuu pamoja na kuwa na ushirikiano na Jumuiya za kimataifa pamoja na Sekta binafsi ili kukabiliana na changamoto ya uendelezaji hasa katika hatua za awali za utafiti ambazo zina gharama kubwa.
Ameongeza kuwa, Tanzania pia inakaribisha mataifa yaliyopiga hatua katika uendelezaji wa jotoardhi kuendeleza Wataalam wazawa katika masuala ya Jotoardhi.
Ndejembi amesema kuwa kutokana na uwepo wa Bonde la Ufa, Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya jotoardhi vinavyoweza kuzalisha megawati 5,000 za umeme. Ametaja kuwa kuna maeneo 52 yenye viashiria vya jotoardhi ndani ya mikoa 16.
Akifungua mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Gauri Singh amesema kuwa nishati ya jotoardhi ni muhimu duniani katika kutoa hakikisho la usalama wa nishati lakini ameeleza kuwa bado mchango wake bado ni mdogo duniani katika kuzalisha umeme hivyo vyanzo zaidi vinapaswa kuendelezwa.
Katika mkutano wa IRENA, Waziri Ndejembi ameambatana na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bakari Ameir, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati.
