Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amewataka Watumishi wa Wizara ya Nishati kuendelea kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ili kufanikisha ajenda hiyo ambayo kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa ajenda ya nishati safi ya kupikia tayari imeanza kuonesha mafanikio nchini na hivyo kupelekea Tanzania kutambuliwa katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo katika nchi zilizo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kamishna Luoga amesema hayo tarehe 18 Machi 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Tatu cha Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati kwa niaba ya Ma-Katibu Wakuu wa Wizara ya Nishati.
“Katika Mkutano wa SADC ambao Tanzania ilishiriki hivi karibuni, kupitia hotuba mbalimbali zilizotolewa katika mkutano huo ikiwemo ya mgeni rasmi ambaye ni Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa aliitambua na kuipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, lakini pia katika maazimio ya mwisho yaliyoandaliwa na sekretarieti ya SADC, nchi zote za SADC zilitakiwa kuunga mkono juhudi hizo za Tanzania.” Amesema Kamishna Luoga
Kutokana na hilo, amempongeza Rais, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazochukua kufanikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia, pia amewapongeza Watumishi Wizara ya Nishati kwa kufanikisha juhudi hizo ambazo zinalenga kuimarisha afya za watanzania na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Aidha, katika kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kilicholenga kujadili, kutoa maoni, ushauri na kupitisha mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2026/2027, Mhandisi Luoga amewataka wajumbe wa Baraza kujiridhisha kuhusu maeneo yote muhimu ya vipaumbele vya Wizara kama yametengewa fedha ili kuwezesha Wizara kuhudumia watanzania kwa ufanisi.
Vilevile, amewataka Watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao na kujiepusha na utoro, rushwa na kutanguliza uzalendo katika kuwahudumia watanzania.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati umehudhuriwa pia na Viongozi wa TUGHE Mkoa na Tawi la Nishati, pamoja wawakilishi kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara














EmoticonEmoticon