WAENDESHA BODABODA BUKOMBE WAAHIDI KUPIGA KURA OKTOBA 29

WAENDESHA BODABODA BUKOMBE WAAHIDI KUPIGA KURA OKTOBA 29

October 08, 2025 Add Comment





*Waomba kushirikishwa mapokezi Dkt. Samia wilayani Bukombe

Waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameahidi kujitokeza na kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja uliofanyika Oktoba 7, 2025 wilayani humo na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko, Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Bukombe, Leonard Mtuta amesema Maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda wapo tayari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni haki yao ya kikatiba.

“ Tuna wanachama 1,445 na sisi tuko tayari kujitokeza kwa wingi ili tupige kura na kuchagua viongozi wetu kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Madiwani wa maeneo yetu,” amesema Mtuta.

Awali, akizungumza na waendesha bodaboda hao Dkt. Biteko amewaeleza umuhimu wa kushiriki kikamilifu kupiga kura na kusisitiza kuwa upigaji kura una uhusiano mkubwa na maisha ya watu sambamba na maendeleo yao, hivyo katu wasipoteze fursa hiyo ya kujiletea maendeleo.

Pia, amewataarifu kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo anatarajiwa kuwepo Wilayani Bukombe Oktoba 12 mwaka huu.

“ Oktoba 12 Mhe. Rais Samia, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi atakuwepo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Igulwa nawaomba sana mshiriki kwa wingi katika mapokezi yake,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa waendesha bodaboda hao wajitokeze kwa wingi kwa kuwa kuna mengi ya kusema wakati wa ziara hiyo.

Aidha, amewahimiza kuungana na kushirikiana na viongozi wa Serikali ili kuweka mkakati wa pamoja wa kujiletea maendeleo.

MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME VITONGOJINI KUKAMILIKA IFIKAPO 2030

October 08, 2025 Add Comment


*📌Huduma ya umeme kwenye vitongoji yafikia asilimia 58*


*📌Majiko banifu 200,000 kuuzwa kwa ruzuku  ya 80% hadi 85% Tanzania bara*


*📌Mitungi ya gesi 452,455 ya kilo 6 kuuzwa kwa ruzuku ya 50%*


*📌Mifumo 20,000 ya umeme jua kufungwa kwa wakazi maeneo ya visiwani*


*📌Serikali kupitia REA kutoa mikopo ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta*


*📌Watumishi REA waipamba wiki ya huduma kwa wateja*


📍Dodoma


Serikali imeeleza mafanikio makubwa ya utekelezaji  wa miradi ya kusambaza umeme maeneo ya vijijini  na pembezoni mwa miji ambapo Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini  (REA) imefanikiwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji vyote 12,318 sawa na asilimia 100 na miradi ya umeme kwenye vitongoji inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.


Mafanikio ya miradi ya umeme Vijijini  yamebainishwa leo Oktoba 8, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini Mha. Jones Olotu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja jijini Dodoma.


"Tanzania bara tuna jumla ya vitongoji 64,359 ambapo kati ya hivyo vitongoji  37,328 sawa na asilimia 58 vimeshafikiwa na huduma ya umeme na bado miradi ya kusambaza na kufikisha huduma ya umeme inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini," Amesema Mha. Olotu. 


Halikadhalika, Mha. Olotu ameongeza kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini unatarajia kukamilisha utekelezaji wa kusambaza umeme kwenye maeneo ya vitongoji ifikapo mwaka 2030 ili watanzania wapate huduma ya umeme ili kukuza maendeleo yao binafsi na uchumi wa Taifa.


Katika hatua nyingine, Mha. Olotu amesema Serikali imepata watoa huduma kwa ajili ya kufungwa mifumo ya umeme jua kwa wakazi wa maeneo ya visiwani Tanzania bara ipatayo 20,000.


Katika hatua nyingine, Mha. Olotu amewaasa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia REA hususan nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kujikinga na madhara ya kiafya,  kimazingira na kiuchumi yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama.


Vilevile, Serikali kupitia REA inaendelea kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kuhifadhi salama bidhaa za mafuta.


Watumishi wa REA wameipamba Wiki ya Huduma kwa Wateja ambayo inafanyika katika ofisi ya Wakala wa Nishati Vijijini makao Makuu jijini Dodoma.


*Mwisho*

WANUFAIKA WA MITAJI YA COOKFUND WAHIMIZWA KUWEKEZA KATIKA MITUNGI MIDOGO YA GESI

October 08, 2025 Add Comment


📌 *Ni mitungi ya kilo tatu au chini ya kilo tatu*


📌 *Lengo ni kuwezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu gharama*


📌 *Wasisitizwa matumizi ya Mita janja (smart meters) ili kuwezesha wananchi kununua gesi kama LUKU.*


Wanufaika wa mitaji kupitia mradi wa CookFund ambao upo chini ya mpango wa kimataifa wa Integrated Approach to Sustainable Clean Cooking Solution unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF)  kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU)  wamehimizwa kuelekeza uwekezaji wao katika uzalishaji na usambazaji wa mitungi midogo ya gesi ya kilo tatu au chini ya kilo tatu ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa urahisi zaidi.




 Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia Wizara ya Nishati,  Nolasco Mlay ameyasema hayo wakati akiendelea na ziara yake jijini Mwanza kwa lengo la kukagua miradi ya Nishati Safi ya Kupikia inayofadhiliwa na Cookfund

ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya nishati safi ya kupikia nchini.


Akiwa jijini Mwanza Mlay aliwatembelea wafanyabiashara wa kuuza gesi walioongezewa mtaji kupitia mradi huo wa CookFund ili kuhakikisha Wananchi wanafikiwa na huduma ya gesi kwa ukaribu zaidi kupitia uinuaji wa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia.


Amesema kupitia Cookfund wafanyabiashara wadogo wanapewa  mitaji na msaada wa kiufundi ili kuongeza wigo wa usambazaji wa majiko bora ya gesi na mitungi ya gesi.


Mlay amewapongeza wanufaika hao wanaouza mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku kwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati na urahisi zaidi huku akizidi kusisitiza kuhusu kuuza pia mitungi ya gesi ya kilo moja hadi tatu.



“Tunahitaji kuona wanufaika wa CookFund wakiwekeza kwenye teknolojia zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Mitungi midogo ni suluhisho linalowezesha watu wengi zaidi kutumia gesi badala ya kuni au mkaa”. Amesema Mlay

Sambamba na hilo,  Mlay ametoa wito kwa wadau wote wa nishati safi ya kupikia kuleta teknolojia ya mita janja (smart meter) kwa baadhi ya maeneo ambayo bado hawana ili kurahisisha ununuzi wa gesi kwa njia ya kidigitali, na kuondoa changamoto za kujaza mitungi kwa gharama kubwa au umbali mrefu.

“Lazima tuhakikishe nishati safi ya kupikia inapatikana kwa bei nafuu, kwa njia rahisi, na kwa vifaa vinavyomfaa kila Mtanzania kwani kupitia teknolojia hii wananchi wataweza kununua nishati hiyo kama wanavyonunua umeme kwa njia ya LUKU ambapo itasaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wa gesi hasa wakati wa kujaza mitungi kwa wananchi wa kipato cha chini”. Amesisitiza Bw.Mlay.


Vilevile amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kubadilika na kutumia nishati safi za kupikia ikiwemo gesi, umeme, mkaa mbadala na bayogesi kwa ajili ya afya bora na mazingira salama.


Kwa upande wao,  Wafanyabiashara wanaouza mitungi ya gesi wamesema kuwa mwitikio kutoka kwa wananchi umekuwa mkubwa  huku baadhi ya wananchi wakikopeshwa mitungi na wengine wakijitokeza kuwekeza kwa kulipa fedha kidogokidogo ili kuweza kupata mitungi hiyo ya gesi  ili kuachana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa afya na mazingira.

UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI WAIMARISHWA KWA TEKNOLOJIA

UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI WAIMARISHWA KWA TEKNOLOJIA

October 07, 2025 Add Comment

 

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile (kulia), akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja uliofanyika leo Oktoba 6,2025  katika ofisi za EWURA jijini Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imerahisisha upatikanaji wa vibali, leseni na utatuzi wa malalamiko kupitia mifumo ya kidijitali, hatua inayowawezesha wananchi kupata huduma popote walipo na kwa wakati bila kulazimika kufika ofisini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja, katika ofisi za EWURA, Dodoma, leo 6.10.2025.

“Tumeendelea kuboresha mifumo yetu ya kidijiti ambayo imeimarisha utoaji wa huduma kwa kasi zaidi na kwa wakati, na kuondoa kabisa malalamiko ya ucheleweshwaji yaliyokuwepo awali” alisema Dkt.Andilile

EWURA inatumia mifumo kadhaa ya kidijiti ikiwamo E- LUC, ambao unasaidia kupokea mrejesho na maoni ya wateja juu ya namna wanavyopokea huduma zinazodhibitiwa kutoka kwa watoa huduma wanaosimamiwa na EWURA. Mfumo huu unapatikana katika aplikesheni ya simu ya kiganjani.

Pia upo mfumo wa LOIS unaorahisisha maombi ya leseni, vibali vya ujenzi wa miundombinu ya bidhaa zinazodhibitiwa pamoja na uwasilishaji wa malalamiko yanayohusu huduma za nishati na maji.

Dkt Andilile amewataka wafanyakazi wa EWURA kuendelea kutoa huduma kwa weledi na kwa wakati ili wateja wake wafurahie zaidi huduma za udhibiti.

 

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile (kulia), akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja uliofanyika leo Oktoba 6,2025  katika ofisi za EWURA jijini Dodoma.

Baadhi ya wafanyakazi wa EWURA wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mkurugenzi Mkuu, Dkt. James Andilile, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja leo  Oktoba 6,2025 .

PPPC YAWANOA MAWAKILI WA SERIKALI UMUHIMU WA PPP KWENYE MIRADI

PPPC YAWANOA MAWAKILI WA SERIKALI UMUHIMU WA PPP KWENYE MIRADI

October 07, 2025 Add Comment

 

MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akizungumza leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akizungumza leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

MKURUGENZI  wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga,akizungumza wakati wa  mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

MKURUGENZI  wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga,akizungumza wakati wa  mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (hayupo pichani),wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

Na Alex Sonna-DODOMA

MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amewataka mawakili wa serikali kuhakikisha maslahi ya taifa yanapewa kipaumbele wakati wa majadiliano na usimamizi wa mikataba ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa Watanzania.

Mhe. Johari ametoa wito huo leo Oktoba 7, 2025, jijini Dodoma, wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili wa serikali kuhusu masuala ya ubia, yaliyoandaliwa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha mawakili wa Serikali  kuelewa kwa kina dhana ya PPP, sheria na mwongozo wake, pamoja na namna bora ya kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema kuwa  mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo mawakili wa serikali kuhusu misingi ya miradi ya ubia, mfumo wa kisheria unaosimamia PPPC nchini, usimamizi wa vihatarishi, majadiliano na usimamizi wa mikataba ya ubia, pamoja na mifumo ya kifedha inayotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Naamini baada ya mafunzo haya, mawakili wa serikali wataimarika katika kushauri, kujadiliana na kusimamia masuala ya kisheria kuhusu mikataba ya PPPC kwa ufanisi, huku wakihakikisha maslahi ya taifa yanabaki kuwa kipaumbele,” amesema Mhe.Johari

Aidha ameongeza kuwa mikataba ya ubia ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa, hivyo ni lazima iandaliwe kwa umakini na kwa kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya nchi.

“Hii itasaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo kuboresha maisha na kuongeza kipato kwa wananchi,” amesisitiza Mhe. Johari.

Hata hivyo amesema kuwa  serikali imeweka misingi madhubuti ya kisheria na kitaasisi kusimamia miradi ya ubia, ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sera na sheria husika, ili kuhakikisha ubia huo unaleta manufaa kwa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka PPPC, Bi. Flora Tenga, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo mawakili wa serikali ili waweze kusimamia mikataba ya ubia kwa ufanisi na kuliepusha taifa na hasara.

“Mwanasheria Mkuu ndiye mwenye jukumu la kutekeleza mikataba ya ubia kwa niaba ya serikali. Hivyo ni muhimu mawakili wake wakapata mafunzo haya ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kulisababishia taifa hasara,” amesema Bi. Tenga.

Aidha ameongeza kuwa mikataba yoyote lazima ipitie hatua stahiki, ikiwemo tathmini ya thamani ya fedha, maandiko ya kisheria na ukaguzi wa kina kabla ya kutiwa saini. Kukosekana kwa mojawapo ya hatua hizo kunaweza kuleta changamoto kubwa.

Naye Mshiriki Moja kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Stanslaus Silayo,ametoa shukrani kwa Kituo cha PPPC kuwapa mafunzo hayo ambayo  yatawasaidia kuingia mikataba yenye tija kati ya serikali na sekta binafsi na kupunguza hatari ya hasara kwenye miradi ya ubia.