*Waomba kushirikishwa mapokezi Dkt. Samia wilayani Bukombe
Waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameahidi kujitokeza na kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja uliofanyika Oktoba 7, 2025 wilayani humo na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko, Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Bukombe, Leonard Mtuta amesema Maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda wapo tayari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni haki yao ya kikatiba.
“ Tuna wanachama 1,445 na sisi tuko tayari kujitokeza kwa wingi ili tupige kura na kuchagua viongozi wetu kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Madiwani wa maeneo yetu,” amesema Mtuta.
Awali, akizungumza na waendesha bodaboda hao Dkt. Biteko amewaeleza umuhimu wa kushiriki kikamilifu kupiga kura na kusisitiza kuwa upigaji kura una uhusiano mkubwa na maisha ya watu sambamba na maendeleo yao, hivyo katu wasipoteze fursa hiyo ya kujiletea maendeleo.
Pia, amewataarifu kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo anatarajiwa kuwepo Wilayani Bukombe Oktoba 12 mwaka huu.
“ Oktoba 12 Mhe. Rais Samia, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi atakuwepo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Igulwa nawaomba sana mshiriki kwa wingi katika mapokezi yake,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa waendesha bodaboda hao wajitokeze kwa wingi kwa kuwa kuna mengi ya kusema wakati wa ziara hiyo.
Aidha, amewahimiza kuungana na kushirikiana na viongozi wa Serikali ili kuweka mkakati wa pamoja wa kujiletea maendeleo.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon