WIZARA YA NISHATI,AfDB WAJADILI UFADHILI WA MRADI WA UMEME WA 400kV KISONGO-SAME-SEGERA

November 04, 2026


DODOMA

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imekutana na ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kujadili uwezekano wa ufadhili wa miradi ya kimkakati ya nishati nchini, ikiwemo ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 (400kV) kutoka Kisongo-Same-Segera.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi inayolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, kuongeza uwezo wa mfumo wa umeme nchini na kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.

Miradi mingine iliyojadiliwa ni pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Lemugur kilichopo mkoani Arusha, pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya kupoza umeme katika maeneo ya Same mkoani Kilimanjaro na Segera mkoani Tanga.

Majadiliano hayo yamefanyika Novemba 4, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma, yakiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, kwa lengo la kujadili mikakati ya upatikanaji wa fedha na maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Luoga amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji, upokeaji na usambazaji wa umeme, akieleza kuwa ongezeko la mahitaji ya nishati nchini linahitaji kuimarishwa kwa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupokea na kupoza umeme, hususan katika maeneo ya Same, Segera na Chalinze.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kusafirisha na kusambaza umeme, sambamba na kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika mikoa ya Arusha na Tanga pamoja na maeneo mengine nchini. 

Katika hatua nyingine, kikao hicho kimejadili namna ya kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo yanayozunguka uwanja wa AFCON jijini Arusha kupitia miundombinu ya kituo cha umeme cha Lemugur, ili kusaidia maandalizi na uendeshaji wa michuano hiyo kwa kutumia huduma ya umeme wa uhakika.

Mbali na uwekezaji katika miundombinu ya umeme, Serikali na AfDB zimejadili uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme (Electric Cooking Appliances), ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Aidha, kikao hicho kimejadili uwezekano wa kufadhili mradi wa kuunganisha umeme kwa zaidi ya kaya 100,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la upatikanaji wa umeme kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 kupitia Mpango wa Mission 300.

Katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na uendelevu, washiriki wamejadili pia upatikanaji wa msaada wa kitaalamu kwa TANESCO, huduma za ushauri elekezi, gharama za uendeshaji pamoja na mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Vilevile, kikao hicho kimeweka msisitizo katika kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa mradi wa 400kV Kisongo-Same-Segera, ikiwemo umuhimu wa kuwashirikisha maafisa wa madawati ya jinsia ili kuhakikisha masuala hayo yanazingatiwa katika hatua zote za utekelezaji.


Suala la fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yataathiriwa na ujenzi wa miundombinu hiyo pia limejadiliwa, likielezwa kuwa linahitaji kushughulikiwa mapema ili kuepusha changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi.


Katika suala hilo, uzoefu wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400kV Nyakanazi-Kigoma umetajwa kuwa mfano wa kuzingatiwa katika kushughulikia fidia kwa wakati, sambamba na kuwawezesha wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka miundombinu ya mradi kupata huduma ya umeme.


Akizungumzia ushirikiano kati ya Serikali na AfDB, Mhandisi Luoga amesema Serikali inathamini mchango wa Benki hiyo katika kufadhili na kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini, akibainisha kuwa bado kuna maeneo mengi yanayohitaji uwekezaji na ufadhili ili kuendelea kuboresha huduma za nishati.


Ameeleza kuwa, kwa kushirikiana na AfDB, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kuzalisha umeme ya Rusumo na Malagarasi, huku mradi wa Kakono ukiwa miongoni mwa miradi inayohusishwa na ushirikiano huo. Miradi mingine ni pamoja na njia za kusafirisha umeme zinazounganisha Tanzania na Kenya, pamoja na Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi kupitia mradi wa Rusumo.


Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, kuimarisha miundombinu ya nishati, kuongeza uwezo wa mfumo wa umeme, kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.


Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »