TANZANIA KUWASILISHA MAFANIKIO YAKE KATIKA ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU JUKWAA LA UMOJA WA MATAIFA

November 04, 2026

GENEVA, Uswisi: Tanzania kesho, Novemba 5, 2026, itakuwa katika jukwaa la kimataifa la haki za binadamu jijini Geneva, itakapowasilisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizotekelezwa katika kuimarisha utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na ustawi wa wananchi, katika Mapitio ya Nne ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Ushiriki huo unaipa Tanzania fursa ya kueleza mbele ya jumuiya ya kimataifa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mapitio yaliyopita, hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na maeneo yanayoendelea kupewa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia falsafa ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs).

Amesema mapitio hayo ni fursa muhimu kwa Tanzania kueleza mafanikio yaliyopatikana, hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo yaliyokubaliwa katika duru zilizopita, pamoja na kuonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha haki za binadamu na ustawi wa wananchi.

Tanzania inashiriki katika duru ya nne ya UPR ikiwa tayari imeshiriki katika mapitio matatu yaliyotangulia mwaka 2011, 2016 na 2021. Katika duru ya tatu, iliyofanyika mwaka 2021, nchi ilipokea mapendekezo 252 kutoka kwa mataifa mbalimbali, ambapo iliridhia mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku 65 yakikosa kuridhiwa.



Tangu mapitio hayo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo yanayogusa ustawi wa wananchi, yakiwemo utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, afya, elimu, upatikanaji wa maji na miundombinu.  Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya haki, usawa wa fursa na maendeleo jumuishi.

Maandalizi ya Taarifa ya Nne ya Kitaifa ya UPR yamehusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mahakama, asasi za kiraia, taasisi za kidini, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine wa haki za binadamu.

Taarifa hiyo inaainisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2026, ikieleza juhudi za kuimarisha mifumo ya haki za binadamu kama msingi wa Maendeleo endelevu

Ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo unaendana pia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa lenye ustawi, haki, ujumuishi na uwezo wa kujitegemea. Dira hiyo inaweka utu wa binadamu, usawa wa fursa na maendeleo ya wananchi katika msingi wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Kwa mantiki hiyo, ushiriki wa Tanzania katika UPR unaunganisha ajenda ya haki za binadamu na malengo mapana ya maendeleo ya Taifa, kwa kuzingatia kuwa upatikanaji wa haki, huduma muhimu na fursa za maendeleo ni mambo yanayochangia ustawi wa wananchi.

UPR ni utaratibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaozipa nchi zote wanachama fursa ya kupitia hali ya haki za binadamu katika nchi zao kwa misingi ya usawa. Kupitia utaratibu huo, nchi huwasilisha taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa, mafanikio na changamoto zilizopo, huku mataifa mengine yakitoa mapendekezo yanayolenga kuimarisha zaidi utekelezaji wa haki za binadamu.

Mapitio ya Nne ya Tanzania yanafanyika katika Kikao cha 53 cha Kikundi Kazi cha UPR kinachoendelea jijini Geneva kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026. Kupitia ushiriki huo, Tanzania inatarajia kuwasilisha hatua ilizochukua katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kuendeleza ushiriki wake katika juhudi za kimataifa za kukuza na kulinda haki za binadamu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »