WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania inaendelea kutambua sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo muhimu za mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa katika kuelekea uchumi shindani unaotegemea maarifa, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuimarisha tafiti, ukuzaji wa teknolojia na ubunifu.
Amesema hayo leo (Jumatano, Novemba 18, 2026) kwenye maadhimisho ya kilele cha miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City.
Akielezea kuhusu mifumo ya data na uratibu, Waziri Mkuu amesema katika dunia ya leo, maendeleo ya sayansi na teknolojia hayawezi kufanikiwa pasipo uwepo wa mifumo madhubuti ya ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na matumizi ya taarifa.
“Ninaipongeza COSTECH kwa kuanzisha na kuendeleza Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISSTI), ambao unaimarisha uratibu wa tafiti za kisayansi nchini na kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi.”
Amesisitiza kuwa mfumo huu unaweka msingi wa kuunganisha watafiti, taasisi za elimu ya juu, wabunifu, watunga sera na wadau wengine katika jukwaa moja la kitaifa. “Kupitia mfumo huu, Tanzania inajenga hazina ya maarifa itakayosaidia kupanga maendeleo kwa misingi ya ushahidi na takwimu sahihi.”
Akitolea mfano, Dkt. Mwigulu alisema zipo bunifu zilizofanywa na vijana ambazo zinatumika kukausha mazao bila kukata miti. “Kwa COSTECH, hii ni miaka 40 ya mafanikio yenye kuleta ufumbuzi kwenye maisha ya kila siku ya Watanzania.”
“Katika maeneo ya vijijini hivi sasa wanatumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na pia wananchi wanatumia mbolea, jambo ambalo zamani lisingeweza kufanyika. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia mwenyewe ameweka msisitizo kwenye matumizi ya sayansi na teknolojia ambapo ameanzisha Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu ili kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu yanageuzwa kuwa bidhaa, huduma na biashara zinazoweza kuleta ajira, kuongeza mapato na kukuza uchumi wa Taifa.”
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau wote waendelee kujenga ubia imara utakaowezesha ubunifu wa Watanzania kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema kuwa na teknolojia bila sayansi ni sawa na kumiliki shamba lakini huwezi kulilima; badala yake unategemea mtu aje alime, avune na kisha aje akugawie.
Pia, Prof. Mkenda amefafanua kuwa Tanzania inapaswa kuwa na vijana wabobezi wa sayansi na teknolojia watakaotumia ujuzi wao kwenye sekta za madini, uchukuzi, miundombinu, afya na kilimo.
Akiwasilisha Maazimio ya Wadau wa Sayansi na Teknolojia kuelekea utekelezaji wa Dira 2050, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonaz, alisema wadau wamekubaliana vipaumbele vya utafiti viendane na mahitaji ya Taifa, uzalishaji, maendeleo ya watu na changamoto za jamii.
“Tanzania ielekeze nguvu na rasilimali katika maeneo machache ya tafiti na teknolojia yenye manufaa makubwa kwa uchumi na wananchi. Fedha za utafiti zisaidie kutatua matatizo yanayowakabili wakulima, wazalishaji na wafanyabiashara.”
Amesisitiza kuwa Dira ya 2050 itafikiwa pale maarifa na teknolojia zitakapoongeza uzalishaji, kufungua ajira na kuboresha maisha ya wananchi.








EmoticonEmoticon