WAZIRI MKUU AIPONGEZA PSSSF KWA KAZI NZURI

November 20, 2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akipokea mkoba wenye machapisho na taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka kwa Afisa Uhusiano Mkuu wa Mfuko huo, Bi. Queen Edward, alipotembelea banda la PSSSF katika Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (Tanzania Real Estate Expo and Forum – TAREX 2026), katika Ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2026.

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza na kuitambua kazi nzuri inayofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), katika kusimamia shughuli zake na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.  

Pongezi hizo amezitoa leo Novemba 20, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (Tanzania Real Estate Expo and Forum – TAREX 2026), yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza wakati akiwa katika banda hilo, Mhe. Dkt. Nchemba aliipongeza PSSSF kwa kazi nzuri inayofanya na kuhimiza kuendelea na juhudi hizo.

“Hongereni sana, natambua kazi nzuri mnayofanya. Endeleeni hivyo hivyo,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Afisa Mwandamizi toka Idara ya Uwekezaji, Milki na Usimamizi wa Majengo wa PSSSF, Bw. Arnold Kagaruki,  ushiriki wa PSSSF katika kongamano na maonesho hayo unatokana na nafasi yake kama mdau muhimu katika sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, kupitia uwekezaji wake katika miradi mbalimbali ya majengo na ardhi nchini.

“ Kuna uwekezaji unaowagusa moja kwa moja wanachama na wananchi kama vile majengo ya kibiashara, nyumba na viwanja; lakini pia Mfuko umewekeza kimkakati ambapo kwa kushirikiana na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, PSSSF imewekeza katika ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre Jijini Arusha ambapo ujenzi umeanza” alisema.

Kongamano na maonesho hayo yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, wakiwemo waendelezaji wa miradi ya majengo, wawekezaji, taasisi za kifedha, mamlaka za udhibiti pamoja na watoa huduma za kitaalamu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Kenya.

Kupitia jukwaa hilo, PSSSF inalenga kuonesha mchango wake katika maendeleo ya sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, kutangaza fursa zinazotokana na uwekezaji wake, kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na Mfuko, Alisema Bw. Kagaruki.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »