
Haijawahi kutokea wanafunzi 90 kupelekwa kusoma nje ya nchi na Serikali kwa wakati mmoja. Kupitia Programu ya Samia Scholarship Extended, vijana hao wanakwenda Algeria kupata maarifa na ujuzi katika fani za sayansi na teknolojia, hatua inayochangia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, na Dira 2050 kwa kujenga rasilimali watu yenye umahiri wa kuchochea maendeleo endelevu.
Akizungumza Novemba 20, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kuwaaga wanafunzi hao, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza kuwa wamechaguliwa kwa ufaulu wao katika masomo ya sayansi kidato cha sita, bila upendeleo. “Mmechaguliwa kwa sababu mmekuwa nyota katika mitihani yenu,” amesema, akifafanua kuwa ufadhili huo si mkopo, bali ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwaendeleza vijana wenye uwezo mkubwa.

Prof. Mkenda amesema uwekezaji katika sayansi na teknolojia unalenga kuijengea Tanzania uwezo wa kuendeleza sekta zake kwa kutumia wataalamu wake. Akitolea mfano reli, ameeleza kuwa kuwa na reli ni maendeleo, lakini kuweza kuijenga wenyewe ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, huku akiwahimiza wanafunzi wengine kusoma kwa bidii ili kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema wanafunzi hao wamebeba matumaini ya Taifa katika kuimarisha uwezo wa nchi kwenye sayansi na teknolojia. Amewataka kuitumia fursa hiyo kujijengea maarifa na ujuzi watakaoutumia kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya Tanzania baada ya kuhitimu masomo yao.
“Mmetumwa na Taifa. Taifa zima limewatuma,” amesisitiza Mhe. Wanu, akiwataka vijana hao kusoma kwa bidii, kutii sheria za Algeria, kudumisha maadili na uzalendo, pamoja na kusaidiana licha ya kwenda katika vyuo tofauti. Aidha, amewaomba wazazi kuendelea kuwashauri na kuwaombea watoto wao ili wakamilishe masomo na kurejea salama kulitumikia Taifa.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema manufaa ya ushirikiano wa elimu kati ya nchi hizo yanaonekana kupitia wahitimu wanaohudumu kama madaktari bingwa, wahadhiri, wahandisi na wataalamu wa TEHAMA nchini na katika kampuni za kimataifa. Amesema mafanikio hayo yanaonesha ubora wa elimu inayotolewa Algeria na umuhimu wa kuendelea kutumia fursa hizo kuandaa wataalamu wanaohitajika kwa maendeleo ya Tanzania.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Ushauri ya Programu ya Samia Scholarship, Prof. Raphael Chibunda, amesema kamati inashirikiana na Wizara pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutafuta nafasi katika vyuo bora duniani. Amewahimiza Watanzania waishio nje ya nchi, hasa wanaofanya kazi katika vyuo na taasisi za kimataifa, kutumia uzoefu na mahusiano yao kusaidia kuongeza fursa za masomo kwa vijana wa Kitanzania.
Akitoa ushuhuda wake, mnufaika wa programu hiyo, Hosea Gideon Ngalama, aliyesoma Shule ya Sekondari Kimamba iliyopo Kilosa, mkoani Morogoro, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwezesha kuendelea na elimu kupitia ufadhili huo. Amejivunia kutoka katika shule ya Serikali na kupata nafasi hiyo, akieleza kuwa inaonesha namna Serikali inavyowajali vijana na kuwawezesha kutimiza ndoto zao za elimu.


EmoticonEmoticon