*📌 Kinatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Afrika Mashariki, kukuza biashara za kikanda na kuongeza fursa za ajira*
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameshiriki hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kuunganisha Magari cha Double Q Automotive Assembly Plant, uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Uzinduzi wa kiwanda hicho umefanyika leo Novemba 19, 2026, katika eneo la Nakirebe, Wilaya ya Mpigi, nchini Uganda, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiviwanda kati ya Tanzania na Uganda.
Kiwanda hicho kinajihusisha na shughuli za kuunganisha na kuzalisha magari ya aina ya SINOTRUK, mradi unaotarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza fursa za ajira, kuimarisha biashara za kikanda na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuweka kipaumbele katika ushirikiano wa viwanda, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kujenga minyororo ya thamani ya kikanda ili kuongeza uwezo wa eneo hilo kushindana katika masoko ya kimataifa.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga uchumi imara wa kikanda, kuongeza uzalishaji na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya hiyo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali za Uganda na Tanzania, wawekezaji, wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda kutoka nchi hizo mbili, pamoja na Mabalozi wa China nchini Tanzania na Uganda.
Aidha, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio (Mafuta na Gesi) na Dkt. Felchesmi Mramba (Umeme na Nishati Jadidifu), pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame wameshiriki katika hafla hiyo.














EmoticonEmoticon