Kampuni ya MKUYU Africa imezindua jukwaa la Miliki Youth Club kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata elimu ya uwekezaji, usimamizi wa fedha na umiliki wa mali, ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.
Jukwaa hilo limekusudiwa kuwakutanisha vijana kutoka vyuoni na maeneo mbalimbali ya kazi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujifunza fursa za kiuchumi na kujenga uelewa kuhusu namna ya kutumia rasilimali walizonazo kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika jukwaa hilo ni namna vijana wanavyoweza kumiliki mali zisizohamishika, kufanya uwekezaji wa muda mrefu na kujenga utajiri kupitia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkurugenzi wa MKUYU Africa, Juneid Othman, aliwahimiza vijana kubadili mtazamo kuhusu mafanikio ya kiuchumi kwa kuanza kufikiria zaidi kuhusu umiliki wa mali na uwekezaji wa muda mrefu.
Alisema vijana wanapaswa kuanza kujenga msingi wa kifedha mapema, hata wanapokuwa bado vyuoni au katika hatua za mwanzo za maisha yao ya kazi, badala ya kusubiri kupata ajira rasmi ndipo waanze kufikiria uwekezaji.
Juneid alieleza kuwa safari yake ya ujasiriamali ilianza akiwa na umri wa miaka 19, wakati akisomea uhasibu, ambapo alianza biashara ya nishati ya jua kwa mtaji wa Sh milioni tatu.
Alisema biashara hiyo ilikua na kupanuka hadi kufikia masoko ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia, kabla ya baadaye kuingia katika sekta ya ujenzi na uwekezaji wa mali isiyohamishika.
Kwa sasa, kupitia uwekezaji wake katika sekta hiyo, Juneid anamiliki mali isiyohamishika zenye thamani inayokadiriwa kufikia zaidi ya Dola za Marekani milioni 30, zikihusisha miradi zaidi ya 10 ya majengo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Dkt. Beatrice Ndung’u, mtaalamu wa biashara, chapa na masoko, alisema kuanzishwa kwa Miliki Youth Club kunalenga kuwapa vijana maarifa na ujuzi utakaowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kutumia fursa zilizopo kujenga ustawi wao wa kiuchumi.
Alisema jukwaa hilo litakuwa sehemu ya kuwajengea vijana uwezo katika masuala ya uwekezaji, usimamizi wa fedha na mbinu mbalimbali za kujenga utajiri kupitia umiliki wa mali.
Uzinduzi wa Miliki Youth Club unakuja wakati vijana wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo ukosefu wa ajira, kipato kisicho na uhakika na uelewa mdogo kuhusu matumizi bora ya rasilimali katika kujenga maisha endelevu ya kifedha.
Kupitia jukwaa hilo, vijana wanatarajiwa kupata fursa ya kujifunza namna ya kupanga matumizi ya fedha, kuweka akiba, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kutambua fursa za uwekezaji zinazoweza kuwasaidia kujenga mali na kuongeza kipato kwa muda mrefu.
Aidha, jukwaa hilo linatarajiwa kuwa kiunganishi cha vijana na wataalamu wa biashara na uwekezaji, pamoja na kutoa nafasi ya kujenga mitandao ya kibiashara, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa yatakayowasaidia kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Mkurugenz wa mkuyu Juneid Othman (wa pili kulia)akiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa MILIKI YOUTH CLUB jijini Dar es salaam
Juneid akifurah na wadau wa MILIKI YOUTH CLUB
EmoticonEmoticon