WANAWAKE 15 WAPATIWA UFADHILI WA MASOMO ENDELEVU KUPITIA MPANGO WA WISE

November 11, 2026


Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Serikali ya Ireland na Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imetoa ufadhili kamili wa masomo ya Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Nishati Endelevu kwa wanawake 15 wa Kitanzania kwa mwaka wa masomo 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya nishati kupitia Mpango wa WISE.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi ufadhili huo iliyofanyika Novemba 11, 2026 katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),  Kamishna Msaidizi  wa Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani, hususan wanawake, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya nishati.

Amesema mpango huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza wataalamu wenye ujuzi katika nishati jadidifu, kuimarisha matumizi bora ya nishati na kuongeza fursa za wanawake kushiriki katika taaluma za kihandisi na nafasi za uongozi ndani ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, amesema Serikali ya Ireland itaendelea kuunga mkono usawa wa kijinsia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia uwekezaji katika elimu na kuwawezesha wanawake kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa kijani.

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, amesema uwekezaji katika elimu ya wanawake una manufaa ya muda mrefu kwa taifa, huku Mkuu wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis Marco Ndomba, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha elimu ya darasani na mafunzo kwa vitendo ili kuwaandaa wahitimu kukabiliana na mahitaji ya sekta ya nishati.

Kupitia ufadhili huo, wanufaika watagharamiwa ada za masomo, posho za kujikimu, bima ya afya, gharama za utafiti na ziara za mafunzo ya kitaalamu. Aidha, watapata fursa za mafunzo kwa vitendo, ulezi wa kitaalamu na kujenga mitandao ya kitaaluma itakayowawezesha kuongeza ujuzi na fursa za ajira.

Mpango wa WISE ulioanza mwaka 2023 umefikisha jumla ya wanawake 60 walionufaika na ufadhili huo, wakiwemo 15 wa mwaka 2026/2027. Mpango huo unaotekelezwa na UNDP kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na DIT unaunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati wa mwaka 2024–2034 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »