Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Tanzania na Algeria zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati kwa lengo la kukuza uwekezaji, kubadilishana uzoefu na kutekeleza miradi yenye manufaa kwa mataifa hayo mawili.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 72 ya Mapinduzi ya Uhuru wa Algeria, iliyofanyika Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, Mhe. Salome amesema sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya nchi hizo, akibainisha kuwa Tanzania inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo unalenga kupanua upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa wananchi, kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu pamoja na kuongeza matumizi ya suluhisho za nishati safi ya kupikia.
Aidha, amesema ushirikiano wa Tanzania na Algeria katika sekta ya nishati unaendana na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, hivyo kuna fursa za kuuimarisha zaidi kupitia kubadilishana uzoefu na uwekezaji wenye manufaa kwa pande zote mbili.
Katika hafla hiyo, Mhe. Salome pia aliwasilisha salamu na pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Rais wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune, Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria.
Kupitia salamu hizo, Rais Samia amewaasa wananchi wa Algeria kuendelea kudumisha amani, umoja, ustawi na maendeleo, huku akisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha urafiki na ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Katika hafla hiyo, Mhe. Salome ameeleza kuwa vita vya ukombozi wa Algeria, vilivyoanza Novemba 1954, vilikuwa chanzo muhimu cha hamasa kwa mataifa mengi ya Afrika katika mapambano dhidi ya ukoloni na kudai uhuru.
Amesisitiza kuwa historia hiyo inaendelea kuwa kumbukumbu muhimu ya mshikamano wa Afrika na umuhimu wa kuendeleza mahusiano ya kindugu, ushirikiano na maendeleo baina ya mataifa ya Afrika.










EmoticonEmoticon