MTENDAJI MKUU WA TEMESA AKAGUA MAENDELEO YA MATENGENEZO YA KIVUKO CHA MV.MAGOGONI NCHINI KENYA

November 25, 2026

 

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Bw. Kheri Mahimbali, amefanya ziara katika Jiji la Mombasa nchini Kenya kwa lengo la kukagua maendeleo ya matengenezo ya Kivuko cha MV. MAGOGONI kinachofanyiwa ukarabati jijini humo.

Akiwa katika eneo la ukarabati, Bw. Mahimbali amekagua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa ukarabati huo na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu kuhusu maendeleo pamoja na kazi zilizobaki kukamilishwa kabla ya kivuko hicho kurejea katika utoaji wa huduma.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), kwa kushirikiana na Mdhibiti wa safari kwa njia ya Maji, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), wamefanya ukaguzi wa pamoja kwa kukagua umbo la kivuko hicho kabla ya kurejeshwa majini kwa ajili ya kuanza majaribio ya mashine na mifumo mingine ya uendeshaji. Ukaguzi huo ulifanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Novemba 2026.

Akizungumzia maendeleo ya ukarabati huo, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi za Vivuko kutoka  TEMESA, Mhandisi. Hassan Karonda, amesema kuwa kazi za ukarabati zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba 2026 na baada ya hapo, kivuko hicho kitafanyiwa majaribio pamoja na ukaguzi wa mwisho utakaofanywa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kabla ya kurejea nchini mapema mwezi Januari 2027.

“Tunatafajia kivuko hiki kirejee katika huduma zake mara tu ukarabati utakapokamilika mwezi Desemba 2027 na kuruhusu majaribio yatakayofanywa na wenzetu wa TASAC.  Na baada ya hapo kivuko kitaanza kutoa huduma eneo la Magogoni Feri kama ilivyokuwa awali kwa ubora zaidi” amesema Mhandisi Karonda”.

Kukamilika kwa matengenezo hayo na majaribio ya mifumo ya uendeshaji kutakuwa hatua muhimu katika kukiwezesha Kivuko cha MV. MAGOGONI kurejea nchini kikiwa katika hali nzuri ya kiutendaji na kuendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa huduma za usafiri majini.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »