TANROADS MBEYA YAJIDHATITI KUIMARISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA

November 22, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya imejipanga kuendelea kuimarisha ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara kwa lengo la kuboresha usafiri na usafirishaji, kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara.

Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora na ya uhakika inayochochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha biashara na kuunganisha maeneo mbalimbali ya uzalishaji na masoko.

Akizungumza kuhusu mikakati hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema wakala huo unaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya barabara kwa kuzingatia viwango vya ubora, thamani ya fedha na muda uliopangwa wa utekelezaji.

Amesema kuwa kwa sasa TANROADS inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara ya Mbeya–Chunya–Makongorosi, ambayo ni sehemu ya mtandao wa barabara ya Mbeya–Chunya–Makongorosi–Rungwa–Itigi–Mkiwa, unaolenga kuunganisha Mikoa ya Mbeya na Singida pamoja na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji.

Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara katika kipande korofi cha Isonje–Njombe ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa wananchi na bidhaa katika maeneo husika. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha mtandao wa barabara, kufungua fursa za kiuchumi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri.

TANROADS imeipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji unaoendelea kufanyika katika ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, akieleza kuwa uwekezaji huo unachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Kwa upande mwingine, TANROADS Mkoa wa Mbeya unaendelea kuhimiza watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, pamoja na kutoa taarifa za changamoto za miundombinu zinazohitaji hatua za haraka za kiufundi.

Kwa upande wao, wananchi wa Mkoa wa Mbeya, Oliver Lameck, Stumai Kabage, Mawazo Mosses, Alpha Mwaisunga, Prosper Mwibabile na Erick Wasua, wameipongeza Serikali kwa uwekezaji katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, wakieleza kuwa hatua hiyo imeleta mabadiliko katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo kurahisisha usafiri, usafirishaji wa mazao na kukuza biashara.

Wamesema uboreshaji wa barabara umeongeza fursa za kiuchumi na kurahisisha mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali, huku ukipunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumiaji wa barabara hapo awali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »