Tarehe 4 Novemba 2026 - Dodoma
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuonesha nafasi yake kama mdau muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia ufadhili wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotoa malighafi kwa viwanda na kufungua fursa za biashara, ajira na uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Ushiriki wa Benki hiyo katika uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Ndogo na Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025) unaonesha umuhimu wa sekta ya kilimo katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya viwanda na biashara nchini.
Uzinduzi wa sera hizo umefanyika tarehe 4 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma, ukiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kupitia uwezeshaji wake wa kifedha, TADB inafadhili shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji, ukusanyaji na uhifadhi hadi uchakataji, usafirishaji na masoko, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya wakulima, wasindikaji na viwanda.
Katika eneo la uongezaji thamani, Benki imewezesha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mafuta ya kula, sukari, asali, mvinyo, unga na mchele, pamoja na shughuli nyingine za uchakataji wa mazao ya kilimo.
Uwekezaji huu unaongeza uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa zinazotokana na malighafi zinazozalishwa nchini, huku ukiongeza mahitaji ya mazao kutoka kwa wakulima na kuwafungulia fursa za masoko.
Hivyo, ufadhili wa kilimo unachangia si tu kuongeza uzalishaji, bali pia kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani.
Aidha, ukuaji wa shughuli hizi unafungua fursa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kushiriki katika biashara zinazohusiana na mnyororo wa thamani, zikiwemo ukusanyaji na ununuzi wa mazao, usafirishaji, uhifadhi, ufungashaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa.
Shughuli hizo pia zinachochea ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuongeza kipato cha wananchi na kupanua fursa za kujiajiri na kuajiri katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa kushiriki katika jukwaa hilo muhimu la kitaifa, TADB inaendelea kuonesha dhamira yake ya kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuchochea maendeleo ya uchumi kupitia uwezeshaji wa kilimo.






EmoticonEmoticon