Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kwa lengo la kuunganisha Mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Kijakazi Yunus Mohamed, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha Mikoa ya Kusini, hususan Lindi, inaunganishwa na Gridi ya Taifa ya Umeme.
Mhe. Salome amesema kuwa miradi hiyo inahusisha ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka Songea hadi Tunduru, Tunduru hadi Masasi na Masasi hadi Mahumbika.
Ameongeza kuwa, sambamba na ujenzi wa njia hizo, Serikali inajenga vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya kilovolti 220/33 vyenye uwezo wa MVA 120 katika maeneo ya Tunduru na Masasi.
Akifafanua hatua za utekelezaji wa miradi hiyo, Mhe. Salome ameeleza kuwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Songea hadi Tunduru umefikia asilimia 51.6 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2027, huku mradi wa Tunduru hadi Masasi ukiwa umefikia asilimia 34 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2027.
Kuhusu mradi wa Masasi hadi Mahumbika, Mhe. Salome amesema kuwa zoezi la uthamini wa mali za wananchi watakaopisha ujenzi wa njia hiyo limekamilika, huku Serikali ikiendelea na malipo ya fidia kwa wananchi walioathiriwa na mradi huo.
Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza ya malipo ya fidia, zaidi ya shilingi bilioni 2.4 tayari zimelipwa kwa wananchi.
Utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwezesha Mikoa ya Lindi na Mtwara kuunganishwa na Gridi ya Taifa ya Umeme.


EmoticonEmoticon