MWIGULU, MKUYU AFRICA WAWATAKA VIJANA KUIJENGA TANZANIA

November 03, 2026

 

Na Mwandishi Wetu, Moscow

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuwa wazalendo na kupenda nchi yao kwa vitendo, hususan kwa kutumia maarifa, ujuzi na fursa mbalimbali katika kuimarisha uchumi na maendeleo ya kiteknolojia nchini.

Dkt. Mwigulu alitoa wito huo wakati wa Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi (Russia–Africa Summit), uliofanyika jijini Moscow, Urusi, ambapo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alipata nafasi ya kukutana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Tanzania walioshiriki mkutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Urusi, uliofanyika pembezoni mwa mkutano huo kwa lengo la kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji katika sekta za nishati, kilimo, madini, ujenzi na miundombinu.

Aliwataka wafanyabiashara hao kutumia maarifa, teknolojia na fursa walizozipata nchini Urusi kuchochea maendeleo ya Tanzania na kujenga uchumi imara unaowezesha vijana kujitegemea badala ya kutegemea ajira pekee.

Miongoni mwa wafanyabiashara vijana walioshiriki mkutano huo ni mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa MKUYU Africa, Juneid Othman, ambaye anaendelea kuwekeza katika maono ya kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika maendeleo ya majengo ya kisasa na miji yenye miundombinu bora barani Afrika.

Juneid ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wanaotumia majukwaa ya kimataifa kutafuta maarifa, teknolojia na washirika wa kibiashara kwa lengo la kukuza uwekezaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

Akieleza mipango yake, Juneid amesema kupitia ushirikiano na wabia mbalimbali katika sekta ya nyumba na ujenzi, wanatarajia kujenga zaidi ya nyumba 3,000 za kisasa kwa ajili ya kuuza na kupangisha katika miji mbalimbali nchini.

Amesema maono yake ni kuona miji ya Tanzania ikipiga hatua katika kuwa na majengo ya kisasa ya makazi na biashara yanayoweza kushindana na miji mikubwa duniani, ikiwemo Dubai, huku yakichangia upatikanaji wa makazi bora na kuboresha mandhari ya miji.

Mbali na sekta ya ujenzi, Juneid amekuwa akishiriki pia katika kupanua fursa za uwekezaji kupitia jukwaa la MILIKI MALI, linalotoa elimu kuhusu mali isiyohamishika na masuala ya fedha, pamoja na Tanzania Brokers Association Board (TBAB), linalolenga kuimarisha taaluma ya udalali na uwazi katika sekta hiyo.

Akizungumza kuhusu ushiriki wake katika mkutano huo, Juneid ameishukuru Serikali kwa kuwapa vijana fursa ya kushiriki majukwaa ya kimataifa kupitia uratibu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Amesema ushiriki huo umewapa fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazoweza kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, pamoja na kujenga mahusiano na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali ambao wanaweza kuleta mitaji na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Chini ya uongozi wa Juneid, MKUYU Africa inalenga kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza Afrika Mashariki katika ujenzi wa miradi mikubwa ya makazi na majengo ya biashara yenye miundombinu ya kisasa.
Mkurugenzi wa MKUYU Afrika Juneid Othman (wa Tatu kushoto) akiwa katika picha Ya pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mwigulu Nchemba baada ya mkutano


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »