Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 28 wa Mwaka wa Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (ECF-SADC) utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 23 Novemba, 2026 hadi 24 Novemba, 2026.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo tarehe 20 Novemba, 2026, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ndg. Ramadhani Kailima amesema mkutano huo wa siku mbili utahudhuriwa na Wenyeviti wa Tume za Uchaguzi 15, Makamishna, Watendaji Wakuu wa Tume za Uchaguzi za ECF-SADC na maafisa waandamizi kutoka katika Nchi wanachama.
Amesema katika mkutano huo mada mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa Tume za Uchaguzi na kuweka mikakati ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwenye uendeshaji wa shughuli mbalimbali za uchaguzi, zitawasilishwa na kujadiliwa.
Ndg. Kailima ameongeza kuwa tukio la ufunguzi wa mkutano huo litatangazwa Mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kurasa za mitandao ya kijamii na amewakaribisha wananchi kufuatilia mkutano huo.
Amezitaja tume wanachama wa ECF-SAC zitakazoshiriki mkutano huo kuwa ni Tume ya Uchaguzi ya Angola (CNE), Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) (CENI), Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Eswatini (EBC), Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho (IEC), Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) na Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Mauritius (ECO).
Tume nyingine ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Tume ya Uchaguzi ya Namibia (ECN), Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC), Tume ya Uchaguzi ya Seychelles (ECS), mwenyeji wa mkutano huo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC), Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC); na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC).
“Umoja huu umeendelea kuziwezesha Tume za uchaguzi kupata fursa ya kuimarisha uwezo wa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi kwa njia ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu kwenye masuala yanayolenga kuboresha, uratibu na usimamizi wa chaguzi”, amesema Ndg. Kailima na kuongeza kuwa:
“Kupitia Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 28 wa ECF SADC tunatarajia Nchi yetu itapata faida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudumisha na kukuza mahusiano ya kikanda na kimataifa, kutangaza vivutio vya utalii, Tume zetu za uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar zitapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na Tume zingine za Uchaguzi.”
Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Management of elections and social media - exploring the role of EMBs in the SADC Region’’, yaani, “Usimamizi wa uchaguzi na mitandao ya kijamii – kubaini wajibu wa Tume za Uchaguzi katika Ukanda wa SADC”.”
Ameongeza kuwa maandalizi yote muhimu kuelekea Mkutano Mkuu wa 28 wa Mwaka wa ECF – SADC yamekamilika, hivyo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatoa wito kwa umma wa Watanzania kujiandaa kuwapokea wageni kutoka nchi wanachama wa ECF-SADC wanaoshiriki mkutano huo wa kihistoria.
ECF-SADC ni jukwaa lililoanzishwa tarehe 27 Julai, 1998 ambalo wanachama wake ni Tume za Uchaguzi za nchi za kusini mwa Afrika. Makao makuu ya Jukwaa hili yapo Mjini Gaborone, Botswana.

EmoticonEmoticon