📌*Utekelezaji wa mradi wafikia asilimia 93 mkoani Lindi*
📌*Kaya 19,700 zafikiwa na kampeni ya kuhamasisha matumizi yenye tija ya umeme na nishati safi ya kupikia*
📌 *REA yaahidi kuongeza kasi ya uunganishaji wa wateja wapya mkoani Lindi*
📍Dar es Salaam
Serikali ya Norway imeonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vitongojini (Hamlet Electrification Project) pamoja na mradi wa Nishati safi ya kupikia mkoani Lindi unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambao umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.
Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 18, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Ushirikiano (Deputy Head of Cooperation) wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Camilla Dannevig, wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy.
Bi. Dannevig ameipongeza REA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Norway, akieleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma ya umeme kwenye vitongoji pamoja na mradi wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mha. Saidy ameishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano na ufadhili wake, akibainisha kuwa uwekezaji huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Aidha, Mha. Saidy amesema REA itaendelea kuongeza kasi ya uunganishaji wa wateja wapya sambamba na kuimarisha kampeni za uhamasishaji ili kuhakikisha wananchi wanatumia fursa zinazotokana na upatikanaji wa umeme katika shughuli za uzalishaji mali, biashara na matumizi ya nyumbani pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amefafanua kuwa kupitia programu ya kuhamasisha matumizi yenye tija ya umeme (Productive Use of Electricity – PUE) na nishati safi ya kupikia (Clean Cooking), REA imetekeleza kampeni ya nyumba kwa nyumba iliyolenga kaya 19,700, ambapo kaya zote zimefikiwa na kuhamasishwa kuunganishiwa umeme na kutumia nishati hiyo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Vilevile, Mha. Saidy ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia teknolojia rafiki kwa afya na mazingira.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira, kulinda afya za wananchi, kuhifadhi misitu na kuchochea matumizi endelevu ya rasilimali za nishati.
Katika hatua nyingine, Mha. Saidy ameihakikishia Serikali ya Norway kuwa REA itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na wananchi wananufaika na uwekezaji uliofanyika.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi wa REA, Mha. Deogratius Nagu, amesema utekelezaji wa mradi wa usambazi wa umeme umefikia asilimia 93, huku kazi zilizobaki zikiendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa. Vile Vile mradi wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia umefikia asilimia 95.
Mradi wa kusambaza umeme unatekelezwa na Mkandarasi M/s Derm Group (T) Ltd, unalenga kupanua upatikanaji wa huduma ya umeme katika vitongoji vya Mkoa wa Lindi, kuchochea shughuli za uzalishaji mali, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Vile Vile mradi wa uhamasishaji wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na matumizi ya umeme katika uzalishaji mali unatekelezwa na M/s Dar Merchant Group,
Utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za REA za kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini na kuwawezesha kutumia nishati hiyo kama nyenzo muhimu ya kujiletea maendeleo endelevu pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuhifadhi mazingira na kuboresha afya.
Mwisho





EmoticonEmoticon