Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Miao Deyu, amewasili nchini Novemba 23, 2026, kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, kupitia majadiliano kuhusu masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja kwa nchi hizi mbili.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Miao alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe akiwa ameambatana na Viongozi wengine kutoka Tanzania na China, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Dkt. Suleiman Haji Suleiman na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian.
Wakati wa ziara hiyo, masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, iliyofanyika mwezi Januari, 2026, maendeleo ya mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.
Aidha, ziara hiyo itahusisha mkutano wa utatu kati ya Tanzania, China na Zambia, utakaotoa fursa kwa nchi hizo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mradi wa TAZARA, ikiwemo utekelezaji wake na nafasi yake katika kukuza biashara, usafirishaji na maendeleo ya uchumi wa kikanda.
Katika kuenzi urafiki na mshikamano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, Mhe. Miao pia atatembelea makaburi ya wataalam wa China yaliyopo Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, kwa heshima ya raia wa China waliopoteza maisha wakati wa kushiriki ujenzi wa Reli ya TAZARA.
Vilevile, atashiriki warsha maalumu kuhusu TAZARA itakayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Kibaha, mkoani Pwani.
Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kuendeleza majadiliano kuhusu masuala ya kipaumbele kwa mataifa hayo mawili, kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango ya pamoja yenye manufaa kwa wananchi wa Tanzania, China na Zambia.
















EmoticonEmoticon