*MOROGORO, Novemba 20, 2026*– Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kuratibu juhudi za kuingiza Elimu ya Bahari (Ocean Literacy) katika mfumo wa elimu nchini kupitia Programu ya Shule za Buluu (Blue Schools Programme), inayolenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa bahari na uhifadhi wa rasilimali zake.
Akifunga warsha ya siku tano katika Hoteli ya Flomi, Morogoro, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Hamisi Masanja Malebo, amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuwajengea vijana maarifa ya kutunza na kutumia rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu.
Warsha hii imewakutanisha wadau kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Elimu Zanzibar na Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam kwa lengo la kuandaa mwongozo wa kuingiza mada za elimu ya bahari katika shule za msingi na sekondari Tanzania Bara na Zanzibar.
Programu hii pia inalenga kuimarisha ushiriki wa walimu, wanafunzi na jamii katika kujifunza kuhusu uhifadhi wa bahari, hususan kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na uvuvi usio endelevu.
Hatua hiyo inaendana na Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na mchango wa bahari katika chakula, ajira, biashara na uchumi wa nchi.
Warsha hii imeungwa mkono na Kamisheni ya Kimataifa ya Oceanografia ya UNESCO (UNESCO-IOC) kupitia Kamisheni Ndogo ya Afrika na Visiwa Jirani (IOCAFRICA).







EmoticonEmoticon