Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), amezihimiza sekta binafsi za Tanzania na India kutumia fursa zinazotokana na kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za ndege za Shirika la Ndege la IndiGo litakalofanya safari zake kati ya Mumbai na Dar es Salaam kuimarisha biashara, kutafuta masoko mapya, kuanzisha ubia na kuvutia uwekezaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa safari hizo jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2026, Mhe. Kihenzile amesema kuimarika kwa mawasiliano ya usafiri wa anga kutachochea ukuaji wa utalii, ukuzaji wa teknolojia, upatikanaji wa ajira na maendeleo ya kiuchumi.
Amewaalika wawekezaji kutoka India kuichukulia Tanzania kama eneo lenye fursa nzuri za uwekezaji na lango la kuingia katika soko la Afrika.
Aidha, amesema safari za Shirika la IndiGo zitakamilisha huduma zinazotolewa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kati ya Dar es Salaam na Mumbai, kwa kuongeza machaguo ya usafiri, ushindani na ufanisi katika sekta ya usafiri wa anga.
Amelikaribisha Shirika la IndiGo nchini na kueleza kuwa mafanikio ya safari hizo yatapimwa pia kwa fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano zitakazozalishwa.
Amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga ili kunufaisha pande zote.








EmoticonEmoticon