Dodoma
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kamisheni ya Nishati ya Afrika (AFREC), imefanya ukaguzi wa upotevu wa umeme katika baadhi ya mifumo ya usambazaji wa nishati hiyo nchini kwa lengo la kubaini changamoto zinazochangia upotevu huo na kuweka mikakati madhubuti ya kuupunguza ili kuongeza ufanisi wa huduma za umeme.
Ukaguzi huo wa wiki moja, umefanyika jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Efficiency First: Powering Africa’s Sustainable Development (2024–2028), unaofadhiliwa na Ufalme wa Denmark na kutekelezwa kwa kushirikiana na AFREC, kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa nishati na kuchochea maendeleo endelevu barani Afrika.
Ukaguzi huo umehusisha wahandisi na mafundi zaidi ya 60 kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na kampuni ya Powerhut kwa ajili ya kukusanya takwimu muhimu za kiufundi na kiutendaji zitakazosaidia kuandaa mipango madhubuti ya uwekezaji na utekelezaji wa hatua za kupunguza upotevu wa umeme katika mifumo ya usambazaji.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya ukaguzi huo kilichofanyika jijini Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Christopher Bitesigirwe, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ufanisi wa matumizi ya nishati nchini, ikiwemo kupunguza upotevu wa umeme katika mifumo ya usambazaji.
Amesema hatua hizo zinaongozwa na Mkakati wa Taifa wa Ufanisi wa Nishati wa mwaka 2024–2034, unaolenga pamoja na mambo mengine kuweka viwango vya chini vya ufanisi wa nishati kwa vifaa, kupunguza upotevu wa nishati na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya nishati.
“Tanzania inatambua ufanisi wa nishati kama nguzo ya kimkakati ya kuimarisha usalama wa nishati, kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi na kujenga sekta ya nishati yenye ustahimilivu na ushindani zaidi. Juhudi hizi zinaonesha dhamira ya Tanzania ya kuongeza thamani ya rasilimali zake za nishati, kupunguza gharama na kusaidia maendeleo endelevu,” amesema Mhandisi Bitesigirwe.
Aidha, amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya nishati barani Afrika, ikiwemo kutekeleza hatua za kimkakati zilizowekwa na Wakuu wa Nchi na Serikali mwaka 2025 kuhusu kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Sera wa AFREC, Mhandisi Nickson Bukachi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo, amesema kupunguza upotevu wa umeme katika mifumo ya usafirishaji na usambazaji ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika, nafuu na endelevu.
Amesema nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na viwango vikubwa vya upotevu wa umeme ikilinganishwa na nchi zilizoendelea, ambazo zinarekodi viwango vya upotevu wa asilimia 6 hadi 10, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha ufanisi wa mifumo ya umeme barani humo.
“Kila uniti ya umeme inayopotea ni fursa iliyokosekana ya kuwasha taa katika nyumba au hospitali, kusaidia biashara au kuchochea ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, kupunguza upotevu huo si kipaumbele cha kiufundi pekee, bali ni hitaji muhimu la kiuchumi na maendeleo,” amesema Mhandisi Bukachi.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na Mkakati na Mpango Kazi wa Ufanisi wa Nishati Afrika (AfEES), uliopitishwa na Mawaziri wa Nishati katika Umoja wa Afrika mwaka 2025, unaolenga kuongeza tija ya matumizi ya nishati barani Afrika kwa asilimia 12 ifikapo mwaka 2030 na asilimia 50 ifikapo mwaka 2050.
Katika ukaguzi huo, wataalamu wamekusanya takwimu za kiufundi na kiutendaji zitakazotumika kuandaa mipango ya uwekezaji na hatua mahsusi za kupunguza upotevu wa umeme katika mifumo ya usambazaji.









EmoticonEmoticon