WANANCHI TARIME WATAKIWA KUTOZUIA UTHAMINI WA MAENEO YA MRADI WA BWAWA LA TSF

October 09, 2026
TARIME, MARA:
Kaimu Mthamini Mkuu wa Serikali, Bw. Chiremeji R. Kome amewataka wananchi ambao maeneo yao yanapisha  mradi wa ujenzi wa Bwawa la TSF la Mgodi wa North Mara wa Barrick kuheshimu katazo lililotolewa na kuacha kufanya maendelezo mapya katika maeneo yao.

Akizungumza wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya zoezi la uthamini katika maeneo hayo Bw. Kome ameeleza kuwa, changamoto kubwa inayojitokeza kwa sasa katika utekelezaji mradi huo ni baadhi ya wananchi kuendelea kufanya maendelezo hata baada ya katazo kutolewa kwa mujibu wa sheria.

“Wananchi hata baada ya katazo bado wanaendelea kufanya maendelezo katika maeneo hayo kwa lengo la kuongeza malipo. Hili ni kinyume na utaratibu na sheria. Tunawasihi waache kufanya hivyo na washirikiane na wataalamu ili zoezi liendelee vizuri,” amesema Kome.

Aidha, Kome amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja.Edward Gowele,  pamoja na viongozi wa Serikali wilayani humo kwa namna wanavyoshirikiana na wananchi kutoa elimu na kusikiliza changamoto zao, akisema ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa wananchi kuelewa umuhimu wa zoezi hilo.

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha wataalamu wanaohusika na uthamini wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, heshima na kwa kuzingatia hali ya wananchi ambao maeneo yao yanahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

“Ni muhimu wataalamu kufanya kazi hii kwa weledi na kuwa na kauli nzuri kwa wananchi, kwa sababu tunatambua kuwa baadhi yao suala la maeneo yao kuchukuliwa linaweza kuwa changamoto kubwa na ndiyo maana kuna timu ya wataalamu wa masuala ya jamii inayotoa elimu kuhusu namna wananchi watakavyoweza kuendelea na maisha baada ya kuhamishwa,” amesema.

Kwa wananchi waliogoma kutoa ushirikiano katika zoezi la uthamini, Bw. Kome amewataka kuelewa kuwa uthamini ni mchakato unaotekelezwa kwa mujibu wa sheria, na kinachopaswa kudaiwa na mwananchi ni fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.

Amesema fidia hiyo inalenga kumwezesha mwananchi kuondoka katika eneo husika na kuendelea na maisha katika eneo jingine bila kupoteza haki yake ya msingi.

“Wananchi washirikiane na wataalamu katika utekelezaji wa zoezi hili na wakubali kulipwa fidia stahiki ili waweze kupisha shughuli za maendeleo. Shughuli hizi si kwa manufaa ya mtu mmoja pekee, bali zina maslahi mapana kwa jamii, ikiwemo ajira na mapato ya Serikali yanayosaidia katika maendeleo ya nchi,” amesema.

Akieleza wajibu wa Serikali katika mchakato huo, Bw. Kome amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Ofisi ya Mthamini wa Serikali ina wajibu wa kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.

“Kazi yetu ni kuhakikisha mwekezaji analipa kile kinachostahili kulipwa na mwananchi naye analipwa kile anachostahili kwa mujibu wa sheria. Hatupaswi kuwa upande mmoja dhidi ya mwingine. Tunachohakikisha ni kwamba haki inatendeka, mwananchi analipwa fidia stahiki na kamili, na mwekezaji analipa kile kinachotakiwa kisheria,” amesema.

Zoezi hilo la uthamini linaendelea katika maeneo yanayohitajika kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Bwawa la TSF la Mgodi wa North Mara, huku Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi, wataalamu, viongozi wa Serikali na mwekezaji ili kuhakikisha mchakato unakamilika kwa kuzingatia sheria na haki za wananchi.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »