PROF. SHEMDOE AWAHIMIZA WANAKATAVI KUTUMIA MAONESHO KUJIFUNZA FURSA ZA KIUCHUMI

October 26, 2026



Na: OWM–TAMISEMI, Tanganyika – Katavi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka wananchi wa Katavi kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi ili kujifunza na kutumia fursa za kiuchumi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda na biashara, pamoja na mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo Oktoba 25, 2026, wakati akizindua rasmi maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Oktoba 25 hadi 31, 2026, katika Viwanja vya Mizengo Pinda Kabungu, wilayani Tanganyika, mkoani Katavi.

“Wananchi wa Katavi, jitokezeni kwa wingi katika viwanja hivi ili kujifunza namna ya kutumia fursa za kiuchumi katika kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda na biashara, pamoja na mikopo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, na kutumia elimu hiyo kuendesha shughuli zenu za uzalishaji na biashara,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Akizungumzia uwezeshaji wananchi kiuchumi, Prof. Shemdoe amesema wananchi watapata fursa ya kujifunza kupitia ushuhuda wa kikundi cha wanawake kilichopata mkopo wa shilingi milioni 15 kupitia asilimia 10 ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika na kufanikiwa kuzalisha mafuta ya mawese na sabuni, hatua iliyowawezesha kupata kipato.

“Akina mama na vijana mliopo hapa, nendeni mkajifunze namna kikundi hicho kilivyoweza kurejesha mkopo na kupata faida iliyowawezesha kununua sare za shule na madaftari kwa watoto wao wanaonufaika na elimu bila ada, huku wengine wakimudu gharama za kuwasomesha watoto wao katika shule binafsi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Ili kuhakikisha maonesho hayo yanaendelea kufanyika kila mwaka, Prof. Shemdoe ameelekeza Viwanja vya Mizengo Pinda Kabungu kuwa eneo rasmi la maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwaunganisha wananchi, wakulima, wafugaji, wachakataji, wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, taasisi za umma na binafsi pamoja na taasisi za kifedha, ili kujifunza teknolojia mpya na za kisasa za uzalishaji na uchakataji, na kuunganishwa na masoko mbalimbali.

Maadhimisho ya Wiki ya Mwanakatavi yalianza mwaka 2022 kufuatia tamko la kimkakati la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeelekeza kila mkoa kufanya maonesho ya wiki baada ya Maonesho ya Nane Nane, kwa lengo la kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu mafunzo na uzoefu uliopatikana.






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »