DC ITUNDA AFUNGA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA MBEYA

October 26, 2026


Na Mwandishi Wetu, Mbeya

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amefunga rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba yaliyofanyika katika Kata ya Itagano jijini Mbeya, ambapo jumla ya wahitimu 47 wamekamilisha mafunzo hayo kwa mafanikio makubwa. 

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wa kina katika masuala ya ulinzi, usalama, uzalendo, pamoja na utumishi uliotukuka kwa Taifa.

Hafla hiyo ya ufungaji wa mafunzo ilifanyika Oktoba 23 2026, katika uwanja wa Shule ya Msingi Itagano jijini Mbeya, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza na wahitimu hao wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Itunda amewataka kutumia vyema maarifa na ujuzi walioupata kwa kuzingatia nidhamu ya hali ya juu, utii wa sheria na uzalendo katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda amani na usalama wa nchi.

Aidha, Mhe. Itunda amesisitiza umuhimu wa wahitimu hao kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuzuia vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi. 

Alieleza kuwa amani na utulivu ndio msingi mkuu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kuvilinda kwa kuimarisha mshikamano, kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu, na kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kuvuruga utulivu katika jamii.

Katika hatua nyingine, Mhe. Itunda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa za Serikali anayoiongoza katika kudumisha amani, utulivu na usalama nchini.

Alibainisha kuwa mazingira salama ndiyo yanayowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.

Akimalizia hotuba yake, Mhe. Itunda amewataka wahitimu hao 47 kuwa mfano bora katika jamii kwa kuzingatia maadili mema, uzalendo na uwajibikaji, huku akiwasihi kutumia mafunzo waliyoyapata kwa manufaa ya jamii nzima na Taifa kwa ujumla.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »