WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na taasisi za dini nchini katika kutekeleza majukumu yao ya kiroho na kijamii kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 4, 2026) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu kwa Kasisi Kanoni Charles Mika Lundu kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Handeni, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme, Chanika, mkoani Tanga.
“Ni azma ya Serikali inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuimarisha ushirikiano na madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini,” amesema.
Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha ushirikiano huo, ikiwemo kubadilisha sheria ili kurahisisha taasisi za dini kupata hadhi ya taasisi za hisani, kushughulikia madeni ya kodi yaliyokuwa yakizisumbua taasisi hizo na kutoa misamaha ya kodi kwa baadhi ya huduma zinazotolewa na taasisi za dini.
“Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi zetu hizi za dini,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea pia kushirikiana na taasisi za dini katika kugharamia sehemu ya gharama za baadhi ya huduma zinazotolewa na taasisi hizo, akisisitiza kuwa milango ya Serikali iko wazi kwa taasisi za dini.
Dkt. Mwigulu pia amewataka wazazi na taasisi za dini kuimarisha malezi ya watoto wa kike na wa kiume, akisema watoto wote wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa familia, jamii na taasisi za dini.
“Kanisa pamoja na wazazi kwa sasa tuweke nguvu sawasawa kwa watoto wote wakike na wakiume kwa sababu kwa sasa wote wako hatarini,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amempongeza Askofu Charles Mika Lundu kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Handeni, akisema anaamini ataendelea kulitumikia Kanisa na jamii kwa uadilifu.
Aidha, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuiombea Tanzania ili amani, utulivu, mshikamano na umoja viendelee kudumu.
“Wanufaika wa amani ni Watanzania wote. Wanufaika wa amani sio Serikali pekee yake. Wanufaika wa amani sio vyama vya siasa pekee yake. Wanufaika wa amani ni Watanzania wote,” amesema.
Dkt. Mwigulu, ambaye leo pia amesimikwa rasmi kuwa Kanoni Mlei wa Kanisa Anglikana Tanzania, alitunukiwa cheo hicho Juni 21, 2026, katika Harambee ya kukamilisha mradi wa jengo la Kitega Uchumi cha Kanisa Anglikana Tanzania, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo la Dodoma.










EmoticonEmoticon