TUMIENI JUKWAA LA KARIAKOO FESTIVAL KUKUZA BIASHARA, UWEKEZAJI, NA UPATIKAJI WA MASOKO YA AFRIKA NA KUSINI MWA AFRIKA - MHE. LONDO

September 25, 2026
-Azindua rasmi msimu wa tatu wa Kariakoo Festival na kuahidi mazingira wezeshi ya biashara

-Awataka wafanyabiashara wa kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi ubora na ushindani

-Asema uchumi wa nchi unategemea mapato, uzalishaji unaozingatia mnyororo wa thamani

Dar es salaam, Septemba 25, 2026

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dennis Londo amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam kutumia fursa ya uwepo wa tamasha la Kariakoo Festival kukuza biashara, uwekezaji na kutumia fursa ya masoko ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kukuza masoko ya bidhaa zao.

Mhe Londo ameyasema hayo leo Septemba 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi tamasha hilo kwa msimu wa tatu na kuongeza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa wa takribani asilimia 70 kufanikisha Dira ya Nchi kwa Mwaka 2050 kwenye eneo la uunganishaji wa biashara na ongezeko la mnyororo wa thamani.

Mhe Londo amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Soko la Kariakoo kwani linachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa nchi, soko la ajira na mzunguko wa fedha na injini ya biashara.

Akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Masoko ya Kariakoo Bw.Jossam Mzava amesema umoja wa wafanyabiashara wa soko hilo umeweza kuwaunganisha wadau wote kwenye sekta ya biashara ndani na nje ya nchi kwa maslahi mapana ya kukuza mapato hapa nchini.

Tamasha hilo lililobeba kaulimbiu ya; 'Bei shwaa shwaaa' ikimaanisha bei imepunguzwa linawakutanisha wafanyabiashara mbalimbali kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali na namna wanavyoweza kutumia masoko ya ndani na nje.

Katika hatua nyingine, Mhe Londo ameziagiza taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuanza kushiriki tamasha hilo ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kupata huduma na elimu juu ya upatikanaji wa leseni, ushindani wa kibiashara na nembo za ubora.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »