MBUNGE Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam Bakari Shingo amewaasa madereva kote nchini kuhakikisha wanarudi darasani kuongeza ujuzi utakaowezesha kuendesha vyombo vya moto kwa usalama zaidi huku wakiwalinda watumiaji wengine wa barabara.
Amesisitiza kuwa kuna tofauti kubwa ya magari ya miaka ya nyuma na sasa hivyo ili kwenda sambamba na kasi ya teknolojia inayotumika kutengeneza magari njia pekee ya madereva kuifanya kazi hiyo kwa weledi na umakini ni kurudi darasani kusoma hakuna njia mbadala.
Mbunge Shingo ameyasema hayo leo Septemba 25,2026 mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea Chuo cha Ufundi Stadi Cha Future World Vocation institute kilichopo Chanika kwa Ndevu jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika chuo hicho pia amepata nafasi ya kuzungumza na mamia ya madereva wanaoendelea na mafunzo ya udereva ili kuuhisha leseni na huku akipata nafasi ya kutembelea Madara mbalimbali yanatukiwa katika kozi zingine zikiwemo za computer Applications,hotel management, Urembo na ususi, Malenzi ya watoto wadogo, na zinginezo.
"Hapa lazima nikiri kuwa nimepata nafasi ya kupata elimu kuhusu masuala ya udereva.Ujue unapokuwa mwakilishi wa wananchi unapata mambo mbalimbali na kuna jambo nililetewa na madereva wenye leseni ya C plain ambao wengi wanaohoji kwanini warudishwe kusoma wakati walipochukua leseni daraja C plain walisoma kozi zote za daraja E,D na waliambiwa kozi zote za madaraja ya chini zimo ndani ya C plain.
“Baada ya kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute Robert Mkolla amenielimisha kuhusu nafasi ya madereva kurudi darasani hivyo nami naungana naye kuwaambia madereva warudi chuo kusoma udereva ili kuuhisha leseni zao lakini pia kuyafahamu kwa undani magari yenyewe jinsi ya kuyaendesha na sheria za usalama barabarani kwa ujumla.”amesema Mbunge Shingo
Akieleza zaidi Mbunge Shingo amesema yeye ni dereva tangu enzi za leseni za vitabu na kwamba magari yaliyokuwa wakiyaendesha wakati ule sio yaliyopo sasa kwani kila siku teknolojia inabadilika na hakuna mahali unaweza kupata teknolojia mpya ya magari yaliyopo zaidi ya chuoni.
Pia amesema amefurahishwa uwepo wa chuo hicho ndani ya Jimbo la Ukonga na hivyo amemuahidi Mkuu wa Chuo hicho kwamba atahakikisha anapeleka vijana wa jimbo hilo kujifunza fani mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.
“Nimekuwa na utaratibu wa kusomesha vijana katika vyuo mbalimbali vya ufundi na mpaka sasa vijana 700 wanaendelea na mafunzo kupitia fedha za mfuko wa Jimbo,fedha za Mbunge pamoja na fedha za marafiki wa Mbunge.
“Hivyo nitazungumza na chuo hiki ili vijana ninaowafadhili wajiunge na masomo kwa ajili ya kupata ujuzi. Mimi hapa nina fani tano na zote nazifanya kwa ufasaha mkubwa na ndio maana kabla ya kuwa Mbunge nilikuwa nimejiajiri,”amesema.
Mhe.Shingo ametumia nafasi hiyo kuwashauri madereva bodaboda nao kuona haja ya kujifunza fani zenye ujuzi kwani udereva bodaboda una mwisho na kwamba uwepo wa chuo hicho maeneo ya Chanika umefanya kiwe karibu na wananchi.
Kuhusu chuo hicho amesema amevutiwa na mandhari mazuri ya kufundishia akitoa mfano kwa madereva wanaojifunza kuendesha magari madogo ndani ya chuo kuna uwanja mkubwa wa kujifunzia kabla ya kutoka nje.
Pia amefurahishwa na uwezo wa walimu wanaofundisha fani mbalimbali katika chuo hicho ikiwemo ya udereva urembo na malezi ya watoto wanatumia mbinu za kisasa za kufundisha huku akitoa rai kwa chuo hicho kutoa kozi zake katika kiwango cha kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute Mkolla amesema amefurahishwa na ujio wa Mbunge Shingo na kwa nafasi yake anayo majukwaa mengi ambayo atayatumia kuelimisha jamii ya wana Jimbo la Ukonga na maeneo mengine kuhakikisha wanapeleka vijana wao katika chuo hicho kupata ujuzi wa fani mbalimbali.
“Tumezungumza na Mbunge kuhusu nafasi yetu kama chuo katika kuhakikisha tunatoa kozi zitakazowezeha vijana wanajiajiri badala ya kusubiria kuajiriwa.Tunaomba ukawe balozi wetu,”amesema na kusisitiza kuna vijana wengi ambao wanamaliza darasa la saba na kidato cha nne ambao badala ya kujiunga na vyuo kupata ujuzi wameamua kuwa dereva bodaboda.
Amesema vijana wanapaswa kufahamu kuwa pamoja na kuwa madereva bodaboda lakini wanayo nafasi ya kusoma na fani nyingine zitakazowezesha kujiajiri .”Hatuwezi kuacha vijana wote wawe waendesha bodaboda lazima tuwashawishi wasome na kozi nyingine kwa ajili ya faida yao na taifa kwa ujumla.” 













EmoticonEmoticon