MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Tanga,Rajabu Abdallah, ametoa Sh milioni 100 kwa ajili
ya ujenzi wa Soko Kuu la Mikinguni, Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga huku akiwaonya
watakaokula pesa hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mweyekiti
huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM wakati wa kukabidhi mfano wa hundi
ya thamani hiyo na kusema kuwa hatomvumilia mtendaji yoyote atakaebainika
kutumia vibaya fedha hizo tofauti na
zilivyotarajiwa.
Aidha alisema kumekuwa na mazoea ya baadhi ya watumishi kutumia vibaya pesa za miradi ya kimaendeleo jambo ambalo linakwamisha maendeleo na kudumaza huduma za kijamii kwa wananchi na kuongeza migogoro baina ya chama na Serikali kwa ujumla.
Fedha hizo ni sehemu ya Sh milioni 300
zinazokadiriwa kugharimu ujenzi wa soko hilo, ambalo linatarajiwa kuanza
kujengwa katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Soko hilo linatarajiwa kuwa miongoni
mwa miradi itakayochochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi na wafanyabiashara
wa Kata ya Mikinguni, huku likitarajiwa kutumia fursa zitakazotokana na ujenzi
wa Barabara ya Tanga–Bagamoyo.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mikinguni, Kijiji cha Stahabu, mara baada ya kukabidhi hundi hiyo, Abdallah aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kusimamia kwa karibu ujenzi wa soko hilo ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema kukamilika kwa mradi huo
kutasaidia kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza fursa kwa wananchi wa
eneo hilo.
“Kazi ya Chama ni kusimamia
Serikali kuhakikisha inatekeleza iliyoyaahidi kwenye Ilani yake. Watendaji
hampaswi kukaa maofisini, tunataka mkatatue kero za wananchi. Mtaalamu yeyote
anayeona Chama kinamfuatilia ajue kabisa Tanga haimfai,” alisema.
AWESO
APIGA STOP MICHANGO MITIHANI
Katika hatua nyingine, Mbunge wa
Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amekabidhi mashine ya kuchapisha
mitihani kwa Shule ya Sekondari ya Mikinguni, ambayo imepewa jina lake.
Aweso alisema amefanya hivyo baada
ya kupata taarifa kwamba wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakichangishwa fedha
kila unapofika muda wa kufanya mitihani.
Alisema suala hilo sasa limetatuliwa
na kupiga marufuku michango hiyo kwa wanafunzi.
Aidha, Aweso alisema atakutana na
wananchi wa Wilaya ya Pangani, hususan wanawake, kujadili namna ya kuwawezesha
kiuchumi ili waweze kukabiliana na changamoto ya mikopo yenye riba kubwa.
“Mmetuchagua tumekuwa viongozi,
tumeona mnavyoumia na mikopo chechefu na kausha damu. Hivi karibuni tutakaa
kikao cha pamoja na kuona namna gani ya kuwezeshana kiuchumi ili mpate faida ya
kutuchagua sisi vijana wenu tuwatumikie,” alisema.
PANGANI
YAFUNGUKA KIUCHUMI
Wilaya ya Pangani inaendelea kupata
miradi mbalimbali inayolenga kuongeza shughuli za kiuchumi, ikiwamo ujenzi wa
Barabara ya Tanga–Bagamoyo.
Mbali na barabara hiyo, zipo pia
mipango ya utekelezaji wa miradi mingine ya uwekezaji, ikiwamo ujenzi wa
kiwanda cha sukari na kiwanda cha madini, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za
biashara na ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo.
mwisho
EmoticonEmoticon