Matumizi ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG) kwenye vyombo vya usafiri yanaendelea kuwavutia wananchi kutokana na manufaa yake ya kiuchumi, huku kilo moja ya gesi hiyo ikiuzwa kwa Shilingi 1,550 pekee.
Hayo yameelezwa na Mjiolojia Nuru Helambili kutoka Wizara ya Nishati wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Helambili amesema matumizi ya CNG husaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri na ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, salama na yenye gharama nafuu kwa wananchi.
Aidha, amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetenga Shilingi bilioni 22.06 katika Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vinavyohamishika vya kujazia gesi asilia (CNG Mobile Stations) vitakavyojengwa katika mikoa ya Dar es Salaam (vituo viwili), Morogoro (kituo kimoja) na Dodoma (vituo viwili).
Amesema ujenzi wa vituo hivyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za CNG nchini na kuchochea matumizi ya nishati hiyo katika sekta ya usafiri.
Wizara ya Nishati inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara na taasisi zake, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu fursa na huduma zinazopatikana katika sekta ya nishati.





EmoticonEmoticon